Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeeleza azma yake ya kuimarisha uwezo wa taifa katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama njia muhimu ya kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Ameeleza kuwa Serikali imepanga kuongeza ufadhili wa miradi ya utafiti na ubunifu kutoka miradi 80 hadi 109, kwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele ya kitaifa. Miradi hiyo inalenga kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchumi wa bluu, uvuvi, maji, kilimo, afya na maendeleo ya viwanda.
Katika hatua nyingine, Serikali kupitia taasisi za elimu ya juu na elimu ya ufundi itatekeleza jumla ya miradi 1,390 ya utafiti katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara, kilimo, uongozi, ushirika, teknolojia, uvuvi, ardhi, mazingira na usanifu majengo. Hatua hii inalenga kuimarisha msingi wa maarifa na ubunifu unaohitajika katika kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, Serikali imepanga kuchapisha jumla ya tafiti 2,497 katika majarida ya kitaifa na kimataifa ili kuongeza usambazaji wa maarifa, kuchochea mijadala ya kitaaluma na kuhakikisha matokeo ya utafiti yanatumika katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Katika kuimarisha miundombinu ya utafiti, Serikali itajenga uwezo wa maabara katika taasisi tano za utafiti na maendeleo ili ziwe maabara za rufaa kwa utafiti wa viwanda na ubunifu wa kisasa. Pia, itaimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, elimu ya juu na sekta ya viwanda ili kuongeza mchango wa sayansi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Serikali pia itaendelea kuhamasisha wabunifu na kuongeza idadi ya wanufaika wanaopata mikopo kupitia Mfuko wa Ubia na Ubiasharishaji wa Ubunifu wa Samia (Samia Innovation Commercialization Fund). Kupitia mpango huo, vyuo vitano vya Maendeleo ya Wananchi vitapatiwa vituo vya ubunifu ili kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.
Katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia, Serikali itaimarisha utafiti na udhibiti wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali. Aidha, itaendelea kukagua vituo 900 vyenye vyanzo vya mionzi na kupima viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 wanaofanya kazi katika mazingira hayo ili kulinda afya za wananchi, wafanyakazi na mazingira.
Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo kuu ya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya viwanda nchini.