Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wabunifu saba nchini wamenufaika na Sh milioni 767 kupitia Mfuko wa Samia Innovation Commercialization Fund unaolenga kusaidia ubidhaishaji wa bunifu na teknolojia za vijana.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027,hatua hiyo inayolenga kuharakisha ubidhaishaji wa bunifu na teknolojia zinazotokana na mawazo ya vijana wa Kitanzania.
Mfuko huo umebainishwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kuunganisha ubunifu na sekta ya biashara, ambapo bunifu mbalimbali zinapewa mtaji wa awali ili ziweze kuingia sokoni na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Serikali itaendelea kuhamasisha wabunifu nchini ili kuongeza idadi ya makampuni na wanufaika wanaopata mikopo kupitia mfuko huo. Lengo ni kuhakikisha mazingira ya ubunifu yanakuwa jumuishi na yanatoa fursa kwa vijana wengi zaidi kushiriki katika maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kisasa.”Amesema Prof.Mkenda
Aidha, katika kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini, Serikali pia itawezesha vyuo vitano vya Maendeleo ya Wananchi kuanzisha vituo vya ubunifu vitakavyotumika kama majukwaa ya kukuza vipaji, kuendeleza mawazo mapya na kuwajengea uwezo vijana katika nyanja za sayansi, teknolojia na ujasiriamali.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ya ubunifu kuwa injini muhimu ya maendeleo ya viwanda na uchumi wa kisasa, huku ikiwapa vijana nafasi ya moja kwa moja kushiriki katika ujenzi wa taifa kupitia ubunifu wao.