Featured Kitaifa

SERIKALI YAVISUKUMA VYAMA VYA USHIRIKA KUJIENDESHA KIBIASHARA

Written by Alex Sonna

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeongeza kasi ya mageuzi katika sekta ya ushirika kwa kuhamasisha vyama kujiendesha kibiashara na kuviunganisha na mifumo rasmi ya kifedha, hatua inayolenga kuvifanya kuwa imara kiuchumi na kuongeza tija kwa wanachama.

Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika utekelezaji wa mkakati huo, Tume kwa kushirikiana na Benki ya Ushirika Tanzania imefanikiwa kuhamasisha vyama vikuu na SACCOS kubwa 52 kuwa mawakala wa benki hiyo, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanachama waliopo maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, vyama vya ushirika 6,545 vimehamasishwa kuwekeza katika Benki ya Ushirika Tanzania, ambapo vyama 1,540 tayari vimewekeza zaidi ya shilingi bilioni 19, ishara ya kuongezeka kwa imani na ushiriki wa wanaushirika katika mifumo rasmi ya kifedha.

Katika kupanua huduma, matawi manne ya Benki ya Ushirika yaliyopo Dodoma, Kilimanjaro, Tabora na Mtwara yanaendelea kutoa huduma, yakitarajiwa kuongeza ujumuishwaji wa kifedha kwa wanachama wa ushirika.

“Serikali imejikita  katika kuongeza thamani ya mazao kupitia ujenzi na ufufuaji wa viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho cha TANECU katika Wilaya ya Tandahimba chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka.”amesema 

Vilevile, juhudi za kufufua viwanda vya kuchakata pamba katika maeneo ya Magu, Manawa na Buyagu zinaendelea, ambapo baadhi ya miradi hiyo imefikia zaidi ya nusu ya utekelezaji. Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza ajira, thamani ya mazao na mapato kwa wakulima.

Katika sekta ya mafuta ya kula, ujenzi wa kiwanda cha Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) umefikia asilimia 90, huku maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nyuzi za kusukia tumbaku katika Wilaya ya Nzega yakiendelea.

Kwa upande wa masoko, Serikali imeendelea kuhamasisha vyama vya ushirika kuuza mazao yao kupitia mifumo rasmi, hususan Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Hadi kufikia Machi 2026, zaidi ya kilo bilioni 1.5 za mazao zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 3.7 zimeuzwa kupitia mfumo huo, hatua iliyoongeza uwazi na kupunguza biashara holela.

Katika kuwajumuisha zaidi vijana na makundi maalum, Tume imefanikiwa kuhamasisha kuanzishwa kwa vyama vya ushirika 25 vinavyoundwa na vikundi vya vijana katika sekta mbalimbali kama kilimo, mifugo, uvuvi, madini na fedha.

Kadhalika, jitihada zinaendelea za kuimarisha ustawi wa wanaushirika kupitia bima na hifadhi ya jamii. Tayari maelfu ya wakulima, hususan wa tumbaku, wamesajiliwa kupata bima ya mazao, huku majadiliano na mifuko ya hifadhi ya jamii yakiendelea ili kupanua wigo wa mafao kwa wanachama.

Katika hatua nyingine, vyama vikuu kadhaa vya ushirika vimeanza kuanzisha SACCOS zao ili kuongeza mitaji na kuwezesha wanachama kupata mikopo yenye riba nafuu, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi vijijini na mijini.

Kwa ujumla, juhudi hizi zinaonesha mwelekeo mpya wa kuifanya sekta ya ushirika kuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi, kwa kuiwezesha kushiriki kikamilifu katika biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma za kifedha kwa wanachama wake.

About the author

Alex Sonna