Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeweka mikakati 30 ya kimkakati inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kuongeza tija na uzalishaji, kuchochea ajira kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mhe.Chongolo amesema Wizara ya Kilimo imejipanga kutekeleza mikakati hiyo katika maeneo manne makuu yanayolenga kubadili taswira ya sekta ya kilimo na kuifanya kuwa injini ya uchumi wa taifa.
Katika kuongeza tija na uzalishaji, Serikali imeelekeza nguvu katika utafiti wa kilimo, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora na miche, pamoja na utoaji wa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu kwa wakulima. Mikakati mingine ni pamoja na usajili wa wakulima, kuimarisha huduma za ugani, kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja na kupima afya ya udongo, pamoja na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na vituo vya huduma za zana za kilimo.
Katika kushughulikia changamoto ya ajira, hususan kwa vijana na wanawake, Wizara imepanga kuimarisha programu ya BBT katika ngazi ya Halmashauri, pamoja na kuwezesha miundombinu ya umwagiliaji kupitia visima vya wakulima wadogo.
Aidha, vijana na wanawake watanufaika na mikopo ya mitaji, uanzishaji wa vitalu vya miche, pamoja na kupewa nafasi ya kushiriki katika uongezaji thamani wa mazao na utoaji wa huduma za ugani kupitia programu za BBT.
Katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe nchini, Serikali imepanga kuwekeza katika miundombinu ya uhifadhi wa chakula ili kufikia uwezo wa kuhifadhi tani milioni 3 ifikapo mwaka 2030. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utaongezewa uwezo wa kununua mazao ya wakulima kwa wingi zaidi.
Serikali pia imeweka mkakati wa kuhamasisha matumizi ya mazao yenye virutubishi ili kukabiliana na changamoto za lishe na udumavu nchini.
Kwa upande wa masoko na mitaji, Wizara imepanga kujenga miundombinu ya masoko ya mazao ya kilimo katika halmashauri mbalimbali, kuimarisha uongezaji thamani kwa kushirikisha sekta binafsi, pamoja na kuongeza mauzo ya mazao ndani na nje ya nchi.
Aidha, Serikali itaongeza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na kuhakikisha maabara za serikali zinafikia viwango vya ubora wa kimataifa ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya dunia.
Kwa ujumla, mikakati hiyo inalenga kuifanya sekta ya kilimo kuwa tegemeo kuu la uchumi, ikichochea ajira, mapato na ustawi wa wananchi katika ngazi zote.