Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha maendeleo ya ushirika pamoja na kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aamesema Wizara ya Kilimo imepanga kutekeleza mikakati mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/2027 inayolenga kufanya sekta ya ushirika kuwa imara zaidi na yenye mchango mkubwa kiuchumi.
Katika kuimarisha maendeleo ya ushirika, Serikali imeelekeza nguvu katika kuboresha ukaguzi na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa uwazi na ufanisi. Aidha, mkazo umewekwa katika kuimarisha ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum, sambamba na kuhamasisha vyama vya ushirika kujiendesha kibiashara kwa tija zaidi.
Kwa mujibu wa mkakati huo, vyama vya ushirika vinatarajiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kujitegemea kiuchumi, kuongeza mapato ya wanachama na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika upande wa TEHAMA, Wizara imepanga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijiti itakayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.
Aidha, Serikali itawekeza zaidi katika mifumo ya kidijiti ili kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto za kiutendaji katika sekta ya kilimo.
Kwa ujumla, hatua hizi zinatarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo na ushirika nchini, kwa kuimarisha uwazi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na rasilimali zilizopo.