Na Mwandishi Wetu
Mbawe Mji Mpya Jogging Club imefanya matembezi ya jogging jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kudumisha amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza asubuhi hii mara baada ya kumaliza matembezi hayo, Mwanzilishi na Mweka Hazina wa klabu hiyo, Bi Rahima Ramadhani Lutinwa, alisema dhamira kuu ya tukio hilo ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kutumia haki yao ya kupiga kura kwa amani na kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Haki ya kupiga kura ni sauti ya mwananchi. Ukikosa kujitokeza kupiga kura, unakuwa umeikosa nafasi ya kuchagua kiongozi sahihi atakayekuwakilisha kwa miaka mitano ijayo,” alisema Bi Rahima kwa msisitizo.
Aidha, alihimiza wananchi wote kuilinda amani ya nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi, akisema amani ndiyo msingi wa maendeleo. “Amani ni urithi wetu sote. Kila mmoja awe balozi wa amani na atimize wajibu wake wa kupiga kura bila vurugu,” aliongeza.
Jogging hiyo imewakutanisha zaidi ya vijana 75 kutoka maeneo ya KunduchiSikansika, ambapo wakiwa wamevalia mavazi maalumu, walibeba mabango yenye jumbe za kuhimiza amani na uwajibikaji wa kiraia. Hata hivyo, Bi Rahima alisema idadi ya washiriki ingekuwa kubwa zaidi kama si ukweli kwamba siku hiyo ilikuwa ya kazi kwa baadhi ya wanachama.
Kwa upande wake, mlezi wa klabu hiyo, Ally Saidi Abdallah Mbawe, alisema wameamua kutumia michezo kama jukwaa la kufikisha ujumbe wa kitaifa.
“Mazoezi ni sehemu ya maisha yetu, lakini leo tumeamua kuyatumia kama njia ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kupiga kura kwa amani,” alisema.
Naye mwanachama wa klabu hiyo, Ezekiel Peter Sedenga, alisema wamekimbia umbali wa zaidi ya kilomita nane kama ishara ya uzalendo na wito kwa Watanzania wote kujitokeza siku ya uchaguzi. “Tunakimbia kwa amani, tunapiga kura kwa amani, tunajenga taifa lenye umoja,” alisema.
Mbawe Mji Mpya Jogging Club imeahidi kuendelea na kampeni za amani na uhamasishaji wa wananchi hadi siku ya uchaguzi, ikisisitiza kuwa kila kura ina maana na kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani ya taifa.










