Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kimataifa ya Societe Generale, Bw. Pierre Palmieri, iliyoshiriki kugharamia mradi wa SGR kipande cha 2 na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni vya SGR, Makuu ya benki hiyo, Jijini Paris, nchini Ufaransa.
Na Benny Mwaipaja, Paris
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa mradi wa treni ya kisasa, SGR, utainufaisha nchi ya Tanzania na nchi nyingine zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kiuchumi na kijamii kwa kukuza biashara na uchumi katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Dkt. Nchemba amesema hayo Jijini Paris nchini Ufaransa, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kimataifa ya Societe Generale, Bw. Pierre Palmieri, iliyoshiriki kugharamia mradi wa SGR kipande cha 2 na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni vya SGR.
Aliishukuru benki hiyo kwa kushiriki katika mradi huo wa kikanda ambao ni wa kimkakati katika kukuza biashara na pia kuonesha nia ya kuendelea kusaidia ujenzi wa SGR unaoendelea ambao kukamilika kwake kutafungua fursa mbalimbali za kiuchumi.
Dkt. Nchemba aliishauri benki hiyo kuangalia maeneo mengine ya kuwekeza nchi Tanzania katika sekta za viwanda, kilimo, nishati, ujenzi wa miundombinu, elimu, afya na pia kushirikiana na sekta binafsi zikiwemo benki za ndani.
Alirejea wito wake kwa Jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Tanzania kwa kuwekeza katika mradi huo wa SGR kwa kutoa huduma za uendeshaji ikiwemo miundombinu ya mabehewa na vichwa vya treni ili kunufaika na soko kubwa la biashara ya treni katika ukanda huo zikiwemo nchi ambazo zinategemea Bandari ya Dar es Salaam, ambazo nchi zao hazipakani na Bahari.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Asociete Generale, Bw. Pierre Palmieri, alisema kuwa benki yake inajivunia kutoa mchango wake katika kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kwa ajili ya mradi huo mkubwa na wa kimkakati kwa nchi ya Tanzania na Ukanda wote wa Afrika.
Bw. Palmieri aliahidi kuwa benki yake itaendelea kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya madini pamoja na ushauri wa kitaalamu katika sekta ya masoko ya mitaji.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kimataifa ya Societe Generale, Bw. Pierre Palmieri, iliyoshiriki kugharamia mradi wa SGR kipande cha 2 na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni vya SGR, Makuu ya benki hiyo, Jijini Paris, nchini Ufaransa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akioneshwa kitu na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kimataifa ya Societe Generale ya Ufaransa, Bw. Pierre Palmieri, iliyoshiriki kugharamia mradi wa SGR kipande cha 2 na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni vya SGR, Makuu ya benki hiyo, Jijini Paris, nchini Ufaransa. katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akiwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kimataifa ya Societe Generale ya Ufaransa, Bw. Pierre Palmieri, iliyoshiriki kugharamia mradi wa SGR kipande cha 2 na ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni vya SGR, Makuu ya benki hiyo, Jijini Paris, nchini Ufaransa. katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Paris, Ufaransa)