Featured Kitaifa

NCHIMBI AWAITA MAMBO YA NDANI ZIARA YAKE KUJIBU MASUALA YA NIDA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amemwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni au naibu wake kuungana nae kwenye ziara mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya uraia, maarufu kama NIDA.

Balozi Nchimbi ambaye yuko katika ziara yake ya siku 6 mkoani Kagera, ametoa maelekezo hayo aliposimama kuwasalimia wananchi wa Kyerwa, katika Uwanja wa Nkwenda Maziwa, akiwa njiani kuelekea Karagwe, leo Alhamis Agosti 8, 2024.

“Tangu nimeanza ziara maeneo ya Mkoa wa Kigoma na hapa Mkoa wa Kagera wananchi wanalalamikia upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA. Hapa pia ninyi kupitia kwa mbunge wenu, Innocent Bilakwate mmelilalamikia.

“Nimeshatolea maagizo mahali pengine mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA uboreshwe na uharakishwe ili wananchi wapate utambulisho wao. Na nimesema wananchi kudai vitambulisho ni dalili ya mapenzi kwa nchi yao,”amesema Balozi Nchimbi.

Baada ya kero hiyo, Balozi Nchimbi aliagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Naibu Waziri ,aungane naye kwenye msafara wake kwa lengo la kutoa ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu vitambulisho vya uraia.

Katika ziara hiyo, yenye malengo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kuhamasisha uhai wa chama na kuwasikiliza wananchi, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Nchimbi ameambatana na Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) – Oganaizesheni, Ndugu Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Ndugu Rabia Hamid Abdalla, Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambapo leo atakuwa Wilaya za Kyerwa na Karagwe.

About the author

mzalendoeditor