Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE: GARI LA WAGONJWA LISITUMIKE KUBEBA NYUMBA NDOGO

Written by mzalendo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene  akikata utepe kwenye gari la wagonjwa huku wananchi wakishuhudia wakati wa makabidhiano ya gari hiyo kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa  katika Kituo cha Afya cha Ipera  kilichopo katika  Jimbo la Kibakwe,  Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene   akizungumza  leo na wananchi wa Kata ya Ipera iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe,  Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ikiwa ni ziara yake ya siku moja ya  kikazi katika Kata hiyo

Sehemu ya wananchi wa Kata ya Rudi iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe,  Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene  , ikiwa ni  ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo Kibakwe

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. George Fuime  akizungumza na wananchi wa Kata ya Ipera iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe,  Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene   kuzungumza nao ikiwa ni  ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  katika Jimbo Kibakwe 

Diwani wa Kata ya Ipera Mhe. Festo Myuguye  akizungumza na wananchi wa Kata ya Rudi iliyopo katika  Jimbo la Kibakwe,  Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma akizungumza na wananchi wake Ipera  wakati wa ziara ya siku moja ya  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene  

Na. Mwandishi Wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe. George Simbachawene ameonya matumizi ya gari  ya wagonjwa (ambulance)  iliyotolewa na Serikali katika Kituo cha Afya cha Ipera lisitumike kubeba nyumba ndogo badala ya itumike  kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa

Pia amesema gari hiyo isitumike  kibiashara kwa kuanza kubeba abiria au mazao bali itumikwe kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hususani akina mama wajawazito

Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kukabidhi gari hiyo mara baada ya kufanya  mkutano wa hadhara  katika  Kata ya Ipera, Kibakwe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma ambapo amewataka wananchi wawe walinzi wa gari hiyo   

‘‘Msisitizo wangu gari hii ya wagonjwa ni gari la Serikali na ni gari ya wananchi hivyo nitawashangaa kuiona gari hii ikibeba abiria au magunia ya mazao, Naombeni kila mmoja wetu awe mlinzi wa gari hii kwani ni yetu sote’’ amesisitiza Mhe.Simbachawene

Amefafanua kuwa azma ya Serikali ya  kutoa gari hiyo ni kuhakikisha inasaidia kuwafikisha wagonjwa katika hospitali ya Rufaa kwa muda muafaka pale ambapo mgonjwa anapewa  rufaa ya matibabu

‘‘ Tunataka tukiliona gari hili likiwa linatembea barabarani liwe limebeba mgonjwa au linaenda kumfuata mgonjwa na sio vinginevyo ’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene  amesema wanaangalia utaratibu wa kuwatafuta madereva wa gari za wagonjwa viliko vituo vya afya  ili magari hayo yasikae makao makuu ya Halmashauri ya  wilaya badala yake magari hayo yakae kwenye maeneo husika  ambako kuna Vituo vya afya

Amesema hali hiyo itasaidia kutoa huduma  ya haraka kwa wagonjwa mara tu pale gari linapohitajika

Aidha,  Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa akina mama wajawazito kuwahi katika vituo vya afya mara waonapo dalili za kuanza kwa uchungu ili kuepuka vifo visivyo vya lazima huku akiwasihi manesi kuwahudumia wagonjwa kwa upendo kama viapo vyao vinavyowataka

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. George Fuime amesema atahakikisha wanafuatilia kwa ukaribu matumizi ya gari hilo ili liweze kuwa  msaada kwa wananchi wote wa Kata ya Ipera na wilaya nzima ya Mpwapwa.

About the author

mzalendo