Featured Kitaifa

MRADI WA LTIP KUMALIZA CHANGAMOTO ZA MAKAZI HOLELA KONDOA

Written by mzalendo

Meneja Urasimishaji Mjini Bw. Leons Mwenda akitoa taarifa fupi ya mradi katika kikao cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Halmashauri ya Mji wa Kondoa tarehe 2Juni 2024 Mkoani Dodoma.

Wadau wa Sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa waliohudhuria Mkutano wa Wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 2Juni 2024 Mkoani Dodoma

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bw. Ally Mbena akifungua kikao cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Halmashauri ya Mji wa Kondoa tarehe 2Juni 2024 Mkoani Dodoma.

Na. Magreth Lyimo, MLHHSD

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umedhamira kumaliza changamoto ya makazi holela kwa kuyafikia maeneo yote ambayo yameendelezwa bila kupangwa na hayajafikiwa na zoezi la urasimishaji katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa.

Mradi huo unalenga kutambua, kupanga, kupima na kuwamilikisha wananchi katika maeneo yatakayofikiwa na mradi pamoja na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi, kutoa elimu ya masuala ya ardhi na kutoa hamasa juu ya usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi.

Hayo yamebainishwa tarehe 24 Juni 2024 na Meneja Urasimishaji Mjini kutoka katika Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Adhi Bw. Leons Mwenda wakati wa ufunguzi wa Kikao cha kujadili utekelezezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Mkoani Dodoma.

Alisema kuwa ni matarajio ya mradi huu kuanza utekelezaji wake mwezi wa tisa mwaka huu ambapo baada ya miezi nane makazi yote yaliyoendelezwa bila kupangwa katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa yatakuwa yamerasimishwa.

‘‘Katika kipindi hiki cha maandalizi tunawaomba viongozi katika maeneo yao waelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kumaliza migogoro ya mipaka na migogoro ya umiliki baina yao ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huu pindi utakapoanza utekelezaji’’ amesema Mwenda.

Aidha alisisitiza ushirikiano wa wadau hasa Waheshimiwa Madiwani na wananchi wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu ya mradi ili kufanikisha malengo ya Serikali kwa kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa kuhakikisha kila kipande kinapangwa, kinapimwa na kumilikishwa.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bw. Ally Mbena amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu utakaotatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao na kuwaomba watendaji wote kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa mradi.  

Mhe. Rachel Sombida Diwani wa Viti Maalumu Kondoa mjini amesema kuwa uwepo wa mradi huu utasaidia katika kuhamasisha wanawake kupata elimu ya masuala ya ardhi itakayopelekea mwamko wa wao kumiliki ardhi.

‘‘Viongozi tukishirikiana na watendaji wa mradi huu elimu sahihi ya umiliki wa ardhi kwa wanawake itatolewa ambayo itapelekea wanawake kujua haki zao katika umiliki wa ardhi lakini pia umiliki wa pamoja baina ya mume na mke’’ amesema Sombida

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umedhamiria kutoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wadau katika ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji.

About the author

mzalendo