Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AAGIZA SHERIA YA NEMC IFANYIWE MABORESHO

Written by mzalendo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.
Na Mwandishi Wetu 
MAKAMU wa Rais, Dk.Philip Mpango amezindua chapisho la utafiti wa hali ya mazingira ya Pwani na Bahari Tanzania Bara huku akiagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuangalia mapungufu ya kisheria yanayosababisha kukosa nguvu katika usimamizi wa usafi wa mazingira ili kufanyiwa marekebisho.
Akizungumza jana kwenye Kongamano la wadau wa mazingira lililoandaliwa na NEMC, Dk.Mpango alisema miji mingi taka zimejaa kila kona na NEMC hawana meno kisheria.
“Tumepiga kelele za kutosha kuhusu usimamizi, utunzaji na usafi wa mazingira na Sheria ni kikwazo basi zitazamwe taratibu zipo, NEMC nendeni mkaangalie Sheria zenu na Taasisi zingine, mnipe mrejesho nijue tatizo ni nini,”alisema.
Alisema kwasasa athari za mabadiliko ya tabianchi zinachangia upotevu wa asilimia moja ya pato la Taifa na inakadiriwa ifikapo Mwaka 2030 kuna uwezekano wa kupoteza asilimia Tatu ya pato la Taifa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Sware Semesi, 
alisema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kwa lengo la kujadiliana namna Bora ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira  ili kutoka na mikakati ya pamoja ya kuzitambua na kushughulikia kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
“Nchi yetu na Dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za kimazingira, mfano mabadiliko ya hali ya hewa, tabianchi, upotevu wa bioanuai, uchafuzi na uharibifu wa mazingira, upungufu wa maliasili, ni ukweli unaoathiri maisha yetu ya kila siku Afya, makuzi, mahusiano, uchumi na madhara haya yatakwenda hadi vizazi vijavyo tusiposhughulikia sasa.”
“Makubaliano ya kisayansi yapo wazi kwamba hatua za haraka na madhubuti zinahitajika ili kulinda mazingira yetu,”alisema 
Alieleza kuwa mazingira ni sekta mtambuka inayohitaji nguvu ya pamoja katika usimamizi wake.
“Baraza lina jukumu la kulinda na kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 na limepewa jukumu la kusimamia athari za mazingira nchini zinazotokana na shughuli za kibinadamu nchini,”alisema.
Alisema usimamizi wa mazingira umeendelea kuhitaji mbinu mpya na za kimkakati kutokana na mabadiliko yanayoendelea kuwepo katika mifumo ya ikolojia na mbinu na teknolojia za uvunaji na uzalishaji.
Alifafanua kuwa katika kuelekea siku ya mazingira duniani Baraza hilo limeona ni muhimu wadau kupata elimu ya mazingira.
“Tunategemea kongamano hili litakuja na njia ya kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuai,”alisema.
Kadhalika, alisema katika kongamano hilo wadau watajadili matumizi ya nishati safi kwa Maendeleo ya nchi na jamii.
“Pia tutajadili uthibiti wa taka ngumu, plastiki na ushiriki wa sekta binafsi katika kuhifadhi mazingira, jambo jingine kupitia kongamano hili ni kuwa na jukwaa mahsusi la wadau wa mazingira nchini ili kukutana kila mwaka kuwa na mikakati yenye tija katika usimamizi wa mazingira nchini,”alisema 
Alisema jukumu la ulinzi wa mazingira si ya Taasisi moja bali ushirikiano wa kila sekta.
“NEMC inathibitisha katika kujitathmini, kujiboresha na kujiimarisha katika kushauri serikali kwenye usimamizi wa mazingira nchini. Leo kutazinduliwa chapisho la hali ya mazingira ya Pwani na Bahari Tanzania Bara ambapo kazi hiyo ilifanyika NEMC kwa kushirikiana na Taasisi zingine,”alisema.
Akiwasilisha maelezo kuhusu chapisho hilo, Dk. Julius Francis kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM alisema ni chapisho la pili kuzinduliwa katika kipindi cha mwezi mmoja na kwamba chapisho la kwanza lilihusu upande wa Zanzibar.
“Chapisho hili limeandaliwa kwa kufuata matakwa ya mkakati wa Taifa wa usimamizi wa rasilimali za Pwani na Bahari, unatoa mchango katika uandaaji wa taarifa ya mazingira na kutimiza matakwa ya mkataba wa kimataifa wa Nairobi katika usimamizi na uendelezaji wa mazingira Bahari na ukanda wa Pwani katika eneo la Bahari ya Hindi kama inavyotakiwa vyombo vingine vya kimataifa kuandaliwa taarifa kila baada ya miaka mitano au 10,”alisema.
Alisema chapisho hilo limeandaliwa na wataalamu 18 kutoka Taasisi za Serikali na limegawanyika katika sehemu kuu sita na mandhari yake ni kuelekea uchumi wa Buluu na mchango wa rasilimali za Pwani na Bahari.
“Chapisho limebeba ujumbe mahsusi katika maeneo manne kuna viashiria vinaonesha baadhi ya makazi ya viumbe yameathirika na yapo hatarini kutoweka iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa ili kurejeshwa katika mazingira ya awali,”alisema 
Mtaalamu huyo alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi maeneo ya Pwani na Bahari zinazotoa fursa ya kujenga uchumi wa Buluu mkubwa na endelevu kw kuunganisha mikakati ya sekta mbalimbali.
“Chapisho hili limekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu ipo kwenye uandaaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na utekelezaji wa sera na mkakati wa uchumi wa Buluu hivyo chapisho hili ni chanzo kizuri cha taarifa za hali ya mazingira na rasilimali za Pwani na Bahari,”alisema 
Alisema katika kujenga uchumi wa Buluu kunahitaji mageuzi ya kimkakati katika kusimamia rasilimali za Pwani na Bahari kwa Kila sekta na mageuzi yanahitaji kufanyika na yatachukua muda matokeo kuonekana.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam kufungua Kongamano la Wadau wa Mazingira tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwandishi wa Vitabu kwaajili ya watoto katika uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Bi. Annastella Mtoka wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

– Advertisement –

Ad image

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha tuzo iliyotolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa katika kulinda na kuhifadhi mazingira iliyotolewa wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024. (Kushoto ni Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi tuzo ya usimamizi mazingira Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Chapisho la Hali ya Mazingira ya Pwani na Bahari ya Tanzania Bara wakati wa Kongamano la Wadau wa Mazingira lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam tarehe 31 Mei 2024.

About the author

mzalendo