Featured Kitaifa

DKT. BITEKO AZINDUA KITUO CHA KUPOZA UMEME IFAKARA

Written by mzalendo

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (katikati) akizindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara ( 20MVA) wilayani Kilombero mkoani Morogoro. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima na kushoto kwake ni Balozi wa Umoja wa Ulaya, Christine Grau

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (katikati) akizungumza mara baada ya kzindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara ( 20MVA) wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

…..

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (20MVA)  ambacho kukamilika kwake kumepelekea  Wilaya za Kilombero,Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro kupata umeme wa kutosha na wa uhakika.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro, Dkt. Biteko amesema kuwa mradi huo una manufaa mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji umeme kwenye wilaya hizo, kuwezesha uwekezaji zaidi wa viwanda hasa vya kilimo kama vile mpunga,
kupeleka huduma kwenye taasisi ikiwemo vituo vya afya na Shule na kuongeza wigo wa gridi ya Taifa.

“ Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inachukulia kwa uzito mkubwa suala la upatikanaji wa nishati kwenye maeneo yetu, wimbo wetu Wizara ya Nishati si kusema maneno mengi bali kupeleka umeme kwa wananchi, umeme kwetu si anasa bali ni jambo la lazima.” Amesema Dkt. Biteko

Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuwezesha mradi huo ulioanza mwaka 2020 ambapo fedha za kutekeleza mradi takriban shilingi Bilioni 25 zimetolewa na Serikali ya Tanzania pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).

Aidha, Dkt. Biteko amewataka Watendaji wa TANESCO na REA kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuweza kufikisha umeme wa uhakika kwa wananchi.

“ Napenda kuwapa hamasa wote mnaohusika na Sekta ya Nishati (REA na TANESCO) kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi hii muhimu itakayochochea kukua kwa uchumi wa watu wetu na niwatake muimarishe usimamizi wa miradi hii ili iendane sawa na thamani ya fedha zinazotolewa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema uwepo wa kituo cha umeme Ifakara unaenda kuchochea uwekezaji ikiwemo ufunguaji wa viwanda 54 vya kuongezea thamani mazao, ujenzi wa migodi mikubwa unaoendelea wilayani Ulanga ambayo ilikuwa ikihitaji umeme wa uhakika ambapo amesema Serikali imeamua kujenga laini ya umeme km 68 kupeleka umeme kwenye migodi hiyo kwa thamani sh. bilioni 104.

katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema Serikali itafungua Ofisi ya TANESCO ngazi ya Mkoa kwenye Kanda ya Morogoro Kusini ili kusogeza huduma zake kwa wananchi badala ya kutegemea kupata huduma kutoka Ofisi ya Mkoa iliyopo Morogoro mjini.

Ameishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa kuiunga Serikali katika utekelezaji wa mradi huo na kuiomba Jumuiya hiyo kushirikiana na Serikali kuongeza transfoma nyingine kwenye eneo la Kituo cha Ifakara ili kuongeza zaidi nguvu ya umeme ambao pia utaingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe.Christine  Grau ameipongeza Wizara ya Nishati,  REA,  TANESCO pamoja na Wakandarasi kwa kukamilisha mradi huo ambao unaenda kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa Tanzania na Umoja wa Ulaya zimekuwa na  ushirikiano wamuda mrefu katika masuala ya Nishati kwa kuwa ndiyo injini katika kuleta maendeleo endelevu na ushirikiano huo umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Nishati Safi ya Kupikia.

Ameeleza kuwa mradi huo wa Ifakara umewezesha wananchi pamoja na taasisi kupata umeme wa uhakika na kwamba wananchi watatumia umeme huo kujiendeleza kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao yao.

Ameahidi kuwa EU itaendele kuiunga mkono Tanzania ya Nishati ili wanannchi wapate Nishati ya uhakika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi ambao unaonekana kwa namna mbalimbali ikiwemo upelekaji wa umeme wa uhakika  kwa wananchi.

Ameongeza kuwa awali wilaya hizo zilikuwa zikipata umeme mdogo na kufanya huduma nyingi kutopatikana kwa ufanisi lakini sasa uwepo wa umeme wa uhakika utapelekea uanzishaji wa viwanda vidogovidogo ikiwemo vya ukoboaji mpunga kwa kuwa eneo hilo ni mzalishaji mkubwa wa mpunga
nchini.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu alisema kuwa, REA ilijenga kituo hicho kutokana na kuwa eneo la kimkakati kutokana na uzalishaji wa mpunga na migodi.

Amesema kuwa jumla ya Wateja 1858 wameungwa na umeme kupitia mradi huo katika vijiji 8 vya Wilaya ya Kilombero, hii ikijumuisha Shule, Zahanati, Vituo vya Afya, Vituo vya Watoto Yatima, Makanisa na Misikiti.

kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Mhe. Aboubakar Asenga ameshukuru kwa uwepo wa kituo hicho pamoja na umeme kufika kwenye vijiji vyote Wilaya ya Kilombero ambapo ameomba umeme huo ufike vitongojini.

About the author

mzalendo