Featured Kitaifa

MCHENGERWA: TUTAZIPIMA HALMASHAURI KWA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI, Zanzibar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kigezo cha ziada ya kuzipima Halmashauri zote nchini kuanzia mwaka wa fedha ujao ni kila Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato kuanzia viwili na kuendelea kwa kila mwaka wa fedha.

Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa kufungua Mkutano wa 38 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa – ALAT Taifa unaofanyika Zanzibar.

Alisema nguvu ya kila Halmashauri ni mapato na ili iweze kutekeleza miradi yenye tija lazima kuwe na mapato ya uhakika.

“Hili tulishalijadili na kamati tendaji ya ALAT na kukubaliana sasa kuanzia mwaka ujao wa fedha kigezo hili kitaingizwa rasmi katika vigezo vya upimaji wa utendaji kazi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa,”alisema.

Aidha Mhe. Mchengerwa alizitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafanya makadirio ya ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia takwimu sahihi za vyanzo vya mapato hivyo kila Halmashauri ina wajibu wa kufanya tathmini ya vyanzo vyake na kubajeti kwa kuzingatia takwimu sahihi.

“Hii tabia ya watu kuweka makadirio y bajeti kidogo na kukusanya zaidi au makadirio juu kisha kukusanya chini sana sio nzuri inaonyesha hakuna takwimu sahihi ya vyanzo vya mapato hivyo bajeti zetu ziendane na uhalisia wa tathmini ya vyanzo vya mapato,” alisema Mchengerwa.

Aliwataka viongozi hao wa halmashauri zote nchini kuzingatia matumizi ya mifumo katika shughuli zote za utumishi, manunuzi ya halmashauri pamoja na ukusanyaji wa mapato.

“Katika usimamizi wa rasilimali watu kuna mfumo wa Usimamizi wa Mishahara (HCIMS) na mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS), Mifumo hii imesaidia kurahisisha kazi na uwajibikaji; Mifumo ya Ununuzi wa Umma (NEST) pamoja na ile ukusanyaji wa mapato kama TAUSI, GoTHOMIS na mingineyo itumike ipasavyo katika Halmashauri zetu.”

“Nitoa onyo kwa Halmashauri yeyote iyakayobainika kuzima mashine za ukusanyaji wa mapato na kukusanya mapato kinyume na utaratibu na kuchepusha mapato hayo amezielekezq kuacha tabia hiyo mara moja kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria,”alisema.

Alisisitiza uadilifu, uchapa kazi na weledi wa hali ya juu katika kuwahudumia wananchi na kuwataka kwenda kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa maono ya Mhe. Rais Samia yanafikiwa.

Awali, akitoa salaam za ALAT Kaimu Mwenyekiti wa ALAT Mhe. Sima Constantine amesema Mkutano huu wa ALAT ni wa 38 na unajumuisha Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri (184), Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya, (184) Wabunge wanaowakilisha Mikoa 26 pamoja na Wawakilishi wa Wanawake katika Serikali za Mitaa (WASEMI).

About the author

mzalendo