Featured Kitaifa

POLISI YAJIPANGA KUIMARISHA ULINZI SIKUKU YA PASAKA WANANCHI WAPEWA TAHADHARI

Written by mzalendo

Na.Abel Paul,Jeshi la Polisi- Arusha.

Jeshi la Polisi Nchini limesema machi 31,2024 Waumini wa Dini za Kikristo wataungana na wenzao Duniani katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka huku likibainisha kuwa limehimarisha ulinzi na usalama kuelekea sikukuu hizo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Naibu kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Sherehe hiyo hutanguliwa na waumini wa dini hizo hukusanyika kwa wingi na kushiriki Ibada ambazo hufanyika nyakati za mchana na usiku,siku za Alhamis,Ijumaa,Jumamosi na Jumapili na Jumatatu ya Pasaka.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kujiimarisha ulinzi na kuhakikisha kwamba ibada na sherehe hizo zinafanyika katika hali ya amani, utulivu na usalama wa kutosha ambapo amebainisha kuwa Jeshi hilo limejipanga kufanya doria katika mitaa na barabara zote kuu ili kuzuia uhalifu au uvunjifu wowote ule wa amani.

Sambamba na hilo amesema katika barabara zote kuu, kutakuwa na doria za Askari ili kuzuia ajali za barabarani, Pamoja na kukagua watakao kiuka sheria za usalama barabarani kama vile kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, wakiwa wamelewa pombe na kujaza abiria kupita kupita kiasi.

Msemaji wa Jeshi hilo amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Viongozi wa nyumba za ibada ambao watakuwa na ibada katika kipindi hiki cha Juma Kuu wasisite kuwasiliana na Viongozi wa Polisi katika maeneo yao ili washirikiane katika kuimarisha usalama kwa kipindi chote.

Vile vile Jeshi hilo Pia linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuzingatia kanuni ya kiusalama inayosema “usalama unaanza na mimi mwenyewe”

Pia Pamoja na hilo Jeshi la Polisi nchini limewataka wananchi kuchukua tahadhari na kujiepusha na marafiki wa mitandaoni na matapeli wanaojitangaza kuwa wanatoa mikopo kupitia mitandao.

About the author

mzalendo