Uncategorized

MTOTO ALIYEKUWA NA TATIZO LA KUMEZA MIAKA SABA AFANYIWA UPASUAJI WA MATUNDU MADOGO KUONDOA KIZUIO

Written by mzalendo

Mwishoni mwa juma lililopita, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilimfanyia upasuaji kwa njia ya matundu madogo (Laparoscopic Hellers Myotomy)mtoto wa miaka saba ambaye alikua na tatizo la kumeza linalojulikana kwa kitaalam kama Achalasia Cardia tangu akiwa na umri wa mwaka moja kutokana na mishipa yake ya fahamu ya koo la chakula kuharibika na kumfanya ashindwe kumeza kwa urahisi.

Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Mbobezi wa Upasuaji wa Matundu Madogo Dkt. Kitembo Kibwana ambaye ameongoza jopo la watalaam wenzake amesema upasuaji huo ulifanyika ili kupunguza kizuizi kati ya umio (koo la chakula) na tumbo na kugawanya safu ya misuli kutoka kwenye umio hadi tumbo ili kumuwezesha mtoto huyo kumeza chakula kwa urahisi.

Dkt. Kibwana amesema Achalasia ni ugonjwa ambao hufanya iwe vigumu kwa chakula na kioevu kupita kutoka koo la kumeza linalounganisha kinywa na tumbo (umio) ndani ya tumbo na kuongeza kuwa tatizo hili hutokana na mishipa kwenye umio kuharibiwa na mwili wenyewe (auto-immune) au baadhi ya maambukizi na kusabaisha umio kupooza na kupanuka kwa muda na hatimaye kupoteza uwezo wa kukamua chakula hadi tumboni na matokeo yake chakula hicho hujikusanya kwenye umio, wakati mwingine huchacha na kurudishwa hadi mdomoni kikiwa na ladha chungu.

Amewataka wananchi wenye changamoto ya kumeza (Achalasia) kufika Hospitali ili kufanyiwa uchunguzi na kisha kupatiwa matibabu stahiki kwani huduma hiyo hutolewa kwa muda mfupi na kumruhusu mgonjwa ndani ya siku angalau mbili kwenda nyumbani kuendelea na shughuli zake.

“Mpaka sasa tumeweza kufanya upasuaji wa aina hii kupitia njia ya matundu (Laparoscopy) kwa wagonjwa wapatao 24 kwa ufanisi mkubwa zaidi ambapo kati ya hai, 3 ni watoto,” ameeleza Dkt. Kibwana.

About the author

mzalendo