Kitaifa

BENKI YA NMB KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Written by mzalendo

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akipokea zawadi kutoka uongozi wa Benki ya NMB, anayekabidhi ni Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Serikali na Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya NMB- Dodoma, Bi Vicky Bishubo walipomtembeela ofisini kwake Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza na baadhi ya viongozi wa Benki ya NMB walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa Benki ya NMB walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.

Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Serikali na Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya NMB Dodoma, Bi Vicky Bishubo akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

NA. MWANDISHI WETU – Dodoma

Uongozi wa Benki ya NMB waahidi kuendelea kuunga mkono shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu katika kuhakikisha wanaimarisha mahusiano yaliyopo na kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuratibu shughuli za Serikali.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Serikali na Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya NMB- Dodoma, Bi Vicky Bishubo wakati walipotembelea na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi pamoja na Naibu wake Bw. Anderson Mutatebwa ofisini kwake Jijini Dodoma.

Alisema kuwa, katika kutoa huduma za kibenki ambazo zinahusu ofisi ya Waziri Mkuu wataendelea kuyafikia makundi mbalimbali ikiwemo vijana kwa kutoa huduma za kibenki popote walipo na hii itasaidia kusukuma juhudi za Serikali katika huduma za kifedha.

“Tumeendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, na hii haitokuwa mwisho tunaahidi kuendelea kufanya hivyo katika kuunga mkono shughuli mnazotekeleza,” alisema Vicky

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi alisema kuwa, Benki ya NMB imefanya jambo muhimu kuitembelea ofisi yake na kueleza namna ilivyojipanga kuhakikisha inaunga mkono shughuli za Serikali na kuwasihi waendelee kufanya hivyo kadiri inavyofaa.

“Ninawapongeza NMB kwa moyo huu na mmetupa kuona umuhimu wa kuimarisha umoja uliopo nitoe wito muendelee kutoa huduma bora za kibenki kwa jamii yetu ili wananchi waendelee kunufaika na uwepo wenu na kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Yonazi

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Anderson Mutatebwa aliwashukuru NMB kwa kuitembelea ofisi hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo bana yao.

About the author

mzalendo