Featured Kitaifa

LTIP YATAMBUA VIPANDE VYA ARDHI 11,000 NZEGA

Written by mzalendo

Kiongozi wa Timu inayotekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Bw. Nolasko Matsuva akielezea namna mradi huo unavyotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora

Meneja Msaidizi wa Urasimishaji Mijini Bw. Martin Orden akitoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Utemini katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora

Afisa Mradi akichukua taarifa muhimu za umiliki kwa mkazi wa Mtaa wa Utemini katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora wakati wa zoezi la kutambua vipande vya ardhi katika mtaa huo

Na Magreth Lyimo, WANMM

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umetambua vipande vya ardhi takribani 11,000 katika Halmashauri ya Mji wa Nzega ikiwa lengo ni kutambua takribani vipande 20,000.

Hayo yamesemwa na Bw. Nolasko Matsuva, Kiongozi wa Timu inayotekeleza mradi huo katika halmashauri ya mji wa Nzega Mkoani Tabora wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa Mradi huo.

‘‘Katika Halmashauri ya Mji wa Nzega utekelezaji wa Mradi ulianza na shughuli za uwandani Desemba 5, 2023 katika Mtaa wa Maporomoko, Uwanja wa ndege, Upiriri, Ushirika, mpaka sasa tuko mtaa wa Nyasa ambapo tumetambua vipande vya ardhi takribani 11,000’’ alisema Matsuva.

Katika mwitikio wa wananchi kushiriki zoezi hilo, Bw. Matsuva amesema wamefanikiwa kutambua vipande 11,000 kwa muda mfupi kwa kuwa walipata ushirikiano mkubwa wa wananchi wa Nzega pamoja na Viongozi wao hatua ambayo imerahisisha zoezi hilo kwenda kwa kasi na ufanisi mkubwa.

Matsuva amesema wananchi wametambua umuhimu wa kupimiwa maeneo na kutoa wito kwa wakazi wa Nzega kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kukamilisha zoezi hilo na kuhimiza kila mmiliki awepo katika eneo lake wakati wa zoezi la utambuzi ili kutoa taarifa sahihi.

‘‘Naishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuuleta mradi huu hapa Nzega, utasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuwa takribani asilimia 99 ya Nzega magharibi na Nzega mashariki itakuwa imepimwa’’ amesema Matsuva.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo katika Halmashauri ya Mji wa Nzega amekiri kuwa mradi huo umewafikia kwa wakati muafaka na utasaidia kuongeza thamani ya maeneo yao pindi watakapomilikishwa Kisheria.

Nae Meneja wa Urasimishaji Mjini Bw. Leons Mwenda amesema mradi huo umedhamiria kutoa takribani hati miliki 1,500,000 katika maeneo ya mjini ambapo mpaka sasa zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kama Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Halmashauri ya Mji wa Nzega, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Shinyanga, Kigoma Ujiji na Halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo jumla ya vipande 50,000 vimetambuliwa katika maeneo hayo kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Januari 2024.

Ameongezea kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuendelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Peramiho.

Aidha, jumla ya Halmashauri 22 zinatarajiwa kuongezwa katika utekelezaji wa mradi huo ifikapo mwezi Aprili mwaka huu ambapo kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji zitafanywa na makampuni binafsi ili kuongeza kasi ya kumfikia kila mlengwa kwa wakati.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unatekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022 – 2027) ambapo lengo lake kuu ni kuongeza usalama wa milki za ardhi nchini.

About the author

mzalendo