Featured Kitaifa

TANZANI NI YA PILI AFRIKA KWA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI – MAJALIWA

Written by mzalendo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua rasmi huduma ya umeme katika kijiji cha Ivugula kulia kwake ni Mhe. Dkt. Francis Michael, Mkuu wa mkoa wa Songwe na kushoto kwake ni Mhe. George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi wakiwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa mkoa wa Songwe pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa mkoa wa Songwe.

……………..

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa  amesema Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini huku akitoa pongezi nyingi kwa Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo, Tarehe 24 Novemba wakati akiongoza hafla ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Ivugula, kata ya Mahenje katika Halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo katika kijiji hicho, jumla ya shilingi milioni 207 zimetumika kufikisha nishati ya umeme huku bilioni 122 zikitumika kutekeleza miradi mitano (5) kwa mkoa wote wa Songwe.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kufikisha huduma mbalimbali katika maeneo ya vijiji ikiwemo huduma ya nishati ya umeme wa uhakika na kusisitiza kuwa umeme ukitumika ipaswavyo; utasaidia kuinua uchumi wa Watu wengi ambao wengi wao, wanaishi vijijini.

“Jukumu moja ambalo sisi, Wasaidizi wa Mheshimiwa Rais alilotupa ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anaishi kwenye nyumba yenye umeme, na agizo hili amelitoa kwetu pamoja na Watu wa REA; wapeleke Wakandarasi vijijini, wapeleke nguzo na nyaya ili kila Mwananchi avute umeme”.

“Mhe. Rais amesema tunapopeleka umeme, tusiangalie aina za nyumba, iwe ni nyumba ya ghorofa, weka umeme, iwe ni nyumba kama hiyo, weka umeme, nyumba ya nyasi, weka umeme na amesema na anataka kusikia Wananchi wa vijijini wanaweka umeme kwa bei nafuu ya shilingi elfu ishirini na saba (27,000/=)”. Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya utekerezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini katika Mkoa wa Songwe; Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti, Mhandisi, Godfrey Chibulunje amesema, Serikali imetenga bilioni 122.7 kwa ajili ya utekerezaji wa miradi mitano ya kusambaza umeme katika vijiji na vitogoji vya mkoa wa Songwe.

Mhandisi Chibulunje ameitaja Miradi hiyo mitano (5) inayotekelezwa katika mkoa wa Songwe kuwa ni pamoja na Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II); Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B (REDPIIB); Mradi wa Kupeleka umeme katika Vitongoji (HEP); Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo; na Mradi wa tano ni wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

“Mkoa wa Songwe una jumla ya vijiji 307 ambapo hadi sasa vijiji 281 sawa na asilimia 91.5% vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini”. Amekaririwa Mhandisi Chibulunje.

Aidha; Mhandisi Chibulunje ameongeza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme vijijini nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa.

Naye Afisa Mpimaji Mwandamizi wa REA; Bwana Hussein Shamdas amesema Wakala upo katika hatua za mwisho katika kukamilisha mfumo wa taarifa wa kijiografia; mfumo utakao kuwa ukitoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini na vitongoji kiditali.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akipokewa na Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti Mhandisi, Godfrey Chibulunje baada ya kuwasili katika kijiji cha Ivagilo, Mbozi mkoani Songwe kwa ajili ya hafla ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji hicho.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA; Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti, Mhandisi, Godfrey Chibulunje akitoa maelezo kwa Mhe. Kassim Majaliwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini mkoani Songwe wakati wa hafla ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji hicho.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti, Mhandisi, Godfrey Chibulunje akitoa maelezo kwa Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini mkoani Songwe kwa kutumia “digital screen”.

Afisa Mpimaji Mwandamizi kutoka REA; Bwana Hussein Shamdas kutoka REA akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kuhusu mfumo wa taarifa wa kijiografia ambao unatoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini na vitongoji kidigitali.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua rasmi huduma ya umeme katika kijiji cha Ivugula kulia kwake ni Mhe. Dkt. Francis Michael, Mkuu wa mkoa wa Songwe na kushoto kwake ni Mhe. George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi wakiwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa mkoa wa Songwe pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa mkoa wa Songwe.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akibonyeza “switch” ili kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Ivugula, wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Mbunge wa Mbozi, Mhe. George Mwenisongole akiwahutubia Wananchi waliokuja kushuhudia tukio hilo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwahutubia Wananchi wa kijiji cha Ivugula waliokuja kushuhudia tukio hilo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwahutubia Wananchi wa kijiji cha Ivugula katika hafla ya kuwasha umeme katika ghala la kijiji hicho.

About the author

mzalendo