Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU ASHTUKIA UPIGAJI FEDHA KIGOMA, AUNDA TIMU YA UCHUNGUZI

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Mjini na Kigoma Vijijini, kwenye ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma Septemba 22, 2023

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalum ya uchunguzi wilayani Kigoma ili ifanye uchunguzi wa fedha zinazopotea kinyemela kupitia mtandao wa watumishi wasio waaminifu.

“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti   kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Septemba 22, 2023) wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini.

Amesema fedha zinazotoka Serikali Kuu huwa zinatumwa na maelekezo mahsusi ya  kwamba zinaenda kufanya shughuli gani; na za makusanyo ya ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na Baraza lote la Madiwani. 

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema Manispaa ya Kigoma ilipokea sh. milioni 500 kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikakaa kwenye akaunti kwa muda mrefu lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya nini.

“Kuna kiasi kingine cha shilingi milioni 447 kilitumwa Kigoma, wakati zinaandaliwa kutoka, Mkurugenzi akazuia. Hongera Mkurugenzi na uendelee kuzizuia, sisi tunamfuatilia Mkurugenzi aliyekuwepo kwa sababu anajua zile shilingi milioni 500 zilitokaje.”

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Waziri Mkuu amesema wao wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo matumizi mabaya ya fedha, makusanyo kidogo sababu ya malumbano, mawakala kukaa na fedha mikononi badala ya kuzipeleka benki, Baraza la Madiwani kukosa taarifa za fedha na kutumia fedha za miradi kulipana posho.

“Kuna watu wamejilipa shilingi milioni 11 zikiwa ni posho ya safari ya Dodoma. Pia wametumia shilingi milioni sita kufanya service ya gari, hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia shilingi milioni 9 kwenye sherehe za Siku ya Mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa shilingi milioni 14. 8 kwenda kwenye sherehe za Nane Nane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?”, alihoji Waziri Mkuu.

Amesema kuna tume ya TAMISEMI ilikwenda kufanya uchunguzi kwenye Halmashauri hiyo kuhusiana na matatizo hayo. Hivyo, ameitaka tume hiyo ikamilishe kazi yake haraka na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi, OR TAMISEMI. “Tume ikamilishe kazi haraka, akabidhiwe Waziri. Namwagiza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa akipokea taarifa ya tume hiyo, aje Kigoma achukue hatua,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa Halmashauri zote mbili waache makundi kwani yanasababisha migongano na kuzorotesha utoaji huduma kwa wananchi. “Migogoro yenu inasababisha upotevu wa rasilimali watu na fedha.”

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma na ameanza ziara ya siku tatu mkoani Kagera. 

About the author

mzalendoeditor