Featured Kitaifa

KIKWETE AWATAKA MAAFISA UTUMISHI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI WALIO KATIKA MAENEO YAO YA KAZI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao

Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na leo wilayani  hapo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe.  Dkt. Vicent Naano  akizungumza kabla ya kumkaribisha  Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzungumza na Watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akiwa akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda  mara baada ya kuwasili  wilayani humo kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili  watumishi hao

Na. Lusungu Helela-Bunda

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaagiza Maafisa Utumishi wa Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake watembelee ofisi za Watumishi zilizopo katika Kata na Vijiji ili kutatua changamoto za watumishi walioko huko.

Aidha, Mhe. Kikwete amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Maafisa Utumishi  kutoa vibali vya kusafiri kwa Watumishi kwenda Jijini  Dodoma katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kufuatilia masuala yao binafsi ya kiutumishi ilhali kazi hiyo ni ya Maafisa Utumishi hao. 

Amesema Watumishi hao hufika Dodoma kwa ajili ya kufuatilia kupandishwa madaraja, kubadilishiwa miundo na kada, kudai malimbikizo ya mshahara, kuwa vitendo hivyo vinawanyima fursa wananchi kuhudumiwa na Watumishi hao waliolazimika kusafiri.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni siku yake ya tatu ya ziara anayoendelea kufanya mkoani Mara ambapo amewataka Maafisa Utumishi hao kuleta matumaini kwa Watumishi wenzao 

“Acheni ile tabia ya kuonekana miungu watu, tatueni matatizo ya watumishi” amesisitiza Mhe.Kikwete.

Amesema Maafisa Utumishi katika Halmashauri hizo ni lazima watambue wateja wao namba moja ni Watumishi wenzao, hivyo ni lazima wawape kipaumbele katika kutatua changamoto zao ili kupata matokeo makubwa.

“Katika ziara zenu mtakazojipangia za kutembelea vituo vya kazi hakikisheni mnatatua changamoto za watumishi wenu huku mkitumia nafasi hizo kwa kuwapatia  taarifa za fursa mbalimbali za kiuchumi na za kujiendeleza kielimu zinazopatikana kwa sasa ” amesema Mhe.Kikwete.

Amesema haipendezi kuona hata masuala madogo tu ya kiutumishi yanayowakabili Watumishi wao yanasubiri hadi siku Waziri au Naibu Waziri atoke Dodoma ndo aje kuyatatua.

Amewaeleza Maafisa Utumishi hao ni lazima wahakikishe utendaji kazi zao unakuwa wa kimkakati na sio kufanya kazi kwa mazoea 

Amesema moja ya jukumu la msingi kwa Maafisa Utumishi ni kuhakikisha Watumishi wanaowaongoza wanatatuliwa changamoto zinazowakabili hata ikibidi kufika Dodoma wasisite kwenda. 

“Maafisa Utumishi hakikisheni mnajipangia ratiba ya kutembelea vituo vyenu zungumzeni na kusikiliza kero za watumishi, sitegemei nikija tena nisikie changamoto ndogo ndogo kutoka kwa watumishi wenu “amesisitiza Mhe. Kikwete.

About the author

mzalendoeditor