Na.ALEX SONNA,MZALENDO BLOG-MANYONI-SINGIDA
MANENO ya uchungu ya Elizabeth Aloyce Ndalo, mkazi wa Kintingo, Lusilile, Kata ya Manyoni,Mkoani Singida yanaeleza hali ngumu anayopitia katika kumlea na kumtafutia matibabu mjukuu wake Priska, ambaye anasumbuliwa na matatizo ya kupumua yanayoendelea kumuweka katika hali ya hatari na kuitia hofu familia yake.
“Unakuta mtoto usiku halali, anahangaika kupumua, anavuta pumzi kwa nguvu. Mimi namwangalia tu huku nikiumia moyoni kwa sababu sina uwezo wa kumsaidia,” anasema Elizabeth kwa uchungu, akielezea hali anayopitia kila anaposhuhudia mjukuu wake akiteseka kutokana na ugonjwa huo.
Elizabeth anasema Priska amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kupumua kwa muda mrefu, hali iliyowalazimu kutafuta huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali kwa matumaini ya kupata suluhisho. Hata hivyo, baada ya jitihada hizo, walielekezwa jijini Dodoma kwa uchunguzi na matibabu zaidi ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Elizabeth, baada ya kufika kwa wataalamu wa afya, waliambiwa kuwa kuna uwezekano mtoto huyo akawa na saratani ya mapafu, hivyo wakashauriwa kufanya vipimo zaidi, ikiwemo uchunguzi wa kinyama (biopsy), ili kuthibitisha hali yake na kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika matibabu.
Hata hivyo, gharama za vipimo na matibabu zimekuwa kikwazo kikubwa kwa familia hiyo, ambayo haina uwezo wa kifedha wa kumudu mahitaji yote ya matibabu. Elizabeth anasema amekuwa akijitahidi kutumia kipato kidogo anachokipata kupitia shughuli mbalimbali ndogondogo, ikiwemo biashara ya kuuza bidhaa, kumhudumia mjukuu wake, lakini hali hiyo imekuwa ngumu zaidi kadiri mahitaji ya matibabu yanavyoongezeka.
Ugumu wa maisha unaomkabili Elizabeth unaongezwa na ukweli kwamba Priska hana malezi ya baba wala mama, hivyo bibi yake ndiye anayebeba jukumu la kumlea, kumtunza na kuhakikisha anapata mahitaji muhimu ya maisha, ikiwemo huduma za afya na elimu. Jukumu hilo limekuwa zito kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi alionao.
Pamoja na changamoto hizo, Elizabeth hajakata tamaa ya kumuona mjukuu wake akipata matibabu na kurejea katika hali yake ya kawaida. Anasema Priska ana ndoto ya kuendelea na masomo kama watoto wengine, lakini kwa sasa hali yake ya kiafya imekuwa kikwazo katika kutimiza ndoto hiyo, jambo linalozidi kumuumiza kama mlezi wake.
Kupitia MZALENDO BLOG, Elizabeth ametoa wito kwa Watanzania wenye moyo wa kujitolea, wadau wa afya, taasisi mbalimbali na watu binafsi kujitokeza kumsaidia Priska kupata vipimo vinavyohitajika na matibabu yatakayoshauriwa na wataalamu wa afya ili kumpa nafasi ya kupambana na hali inayomkabili.
Anasema msaada wowote utakaotolewa utakuwa na maana kubwa katika safari ya matibabu ya mtoto huyo, ambaye kwa sasa anahitaji mshikamano wa jamii ili kupata huduma za afya ambazo familia yake imeshindwa kuzimudu kutokana na hali ngumu ya maisha.
WATANZANIA WANAWEZA KUMSAIDIA PRISKA KUPITIA MAWASILIANO YAFUATAYO:
-
Jina: Elizabeth Aloyce Ndalo
-
Simu: 0768 251 151
Priska anahitaji nafasi ya kupata matibabu na kuendelea na ndoto yake ya elimu. Msaada wako unaweza kuwa sehemu ya matumaini mapya katika maisha yake.