Featured • Kitaifa

MTWALE AWATAKA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI KUZINGATIA MUDA, USAHIHI WA TAARIFA ZA UTEKELEZAJI WA ILANI

Written by Alex Sonna

 

 

Na OWM-TAMISEMI, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Bw. Sospeter Mtwale, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa (Sehemu ya Mipango na Uratibu) kutambua wajibu wao, kuzingatia muda na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupitia na kuandaa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Bw. Mtwale ametoa wito huo leo Novemba 11, 2026, wakati akifungua Kikao Kazi cha kupitia na kuandaa kwa pamoja taarifa za utekelezaji wa Ilani katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Glonency jijini Dodoma.

Amesema kuwa ushiriki wa kila mshiriki ni muhimu katika kuhakikisha taarifa zinazokusanywa zina ubora unaohitajika, zinakuwa na takwimu sahihi, ushahidi wa kutosha na zinaakisi hali halisi ya utekelezaji katika maeneo yao.

“Ndugu washiriki, nasisitiza mambo manne; kila mmoja atambue wajibu wake, tuzingatie muda, taarifa hizi ziwe za ukweli, sahihi na zenye ushahidi wa kutosha, na tushiriki kikamilifu ili tuweze kukamilisha kazi hii kwa wakati, kwani ucheleweshaji unaweza kuathiri maandalizi ya vikao vinavyotegemea taarifa hizi,” amesema Bw. Mtwale.

Aidha, amesema kuwa kukamilika kwa taarifa hizo za kuanzia kipindi cha Novemba 2025 hadi Oktoba 2026 kutaiwezesha Serikali kupata picha ya utekelezaji katika mikoa, kubaini matokeo yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuimarisha utoaji wa huduma na ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa OWM-TAMISEMI itaendelea kushirikiana kwa karibu na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kwa kuwajengea uwezo katika kuandaa, kupitia na kuboresha taarifa hizo, hatua itakayosaidia kuimarisha uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika ngazi ya mikoa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Tawala za Mikoa kutoka OWM-TAMISEMI, Bw. Johnson Nyingi amesema kuwa kikao kazi hicho kinalenga kuunganisha nguvu na utaalamu wa washiriki katika kuandaa taarifa ya pamoja ya utekelezaji wa Ilani kwa kipindi husika, ili kuhakikisha taarifa inayowasilishwa inakuwa na takwimu zinazolingana, sahihi na zinazoweza kutumika katika kufanya tathmini na maamuzi ya kiutendaji.

About the author

Alex Sonna