Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ASHIRIKI MKUTANO WA DHARURA SADC 

Written by mzalendoeditor

Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ahudhuria Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Organ Troika, SADC Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi katika Force Intervention Brigade (FIB) Windhoek nchini Namibia.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan  amehudhuria Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa nchi ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Mkutano huo wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force  Intervention Brigade (FIB) umefanyika leo mjini Windhoek nchini Namibia. 

Aidha, mkutano huo umetoa tena wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama  na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.  

Mkutano huo pia umewasihi wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC  na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya Uchaguzi  Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2023. 

Vile vile mkutano huo umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano  dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo ili kuleta amani endelevu,  usalama na ustawi kwa wananchi wa Kongo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla. 

Kwa upande mwingine, mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la  SADC kutoka katika Kikosi cha Kudumu cha Jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC  iweze kurejesha amani na usalama.  

Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa  Namibia Mhe. Dkt. Hage Geingo; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Rais  wa DRC Mhe. Félix Antoine Tshisekedi; Waziri wa Mahusiano ya Mambo ya Nje wa  Jamhuri ya Angola Mhe. Balozi Téte António; Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Malawi  Mhe. Harry Mkandawire; pamoja na Balozi wa Zambia nchini Namibia Mhe. Stephen  Katuka. 

About the author

mzalendoeditor