Featured Kitaifa

CHIKOTA:NANYAMBA KUNA UPUNGUFU WA WATUMISHI WA AFYA 610

Written by mzalendoeditor

 

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

SERIKALI imeombwa kupeleka watumishi wa kada za afya kwenye Halmashauri zinazokabiliwa na uhaba mkubwa ikiwamo Halmashauri ya Mji wa Nanyamba yenye upungufu wa watumishi wa kada hiyo 610.

Akiuliza maswali bungeni leo, Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdullah Chikota, amesema upungufu watumishi huo upo kwenye Kituo Cha Afya Majengo, Jinyecha, Kilomba na Hospitali ya Halmashauri hiyo.

“Serikali Ina mpango gani wa dharura wa kupunguza tatizo la watumishi Nanyamba. pia Wizara ya Afya imetoa mwongozo wa wanafunzi waliomaliza masomo kada za afya wajitolee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, je serikali haioni ni wakati muafaka wa kutenga fedha kwasasa waanze kufanya kazi kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa,”amesema.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk.Festo Dugange, amekiri kuwapo na upungufu huo na kwamba mpango wa serikali ni kuajiri na kupeleka kwenye maeneo yenye upungufu.

“Nikuhakikishie katika ajira zilizotangazwa Halmashauri zenye upungufu mkubwa zitapewa kipaumbele,”amesema.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kupeleka watumishi na vifaa tiba katika Kituo cha Afya Majengo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema katika miaka mwili ya mwaka 2020/21 na 2021/2022 Serikali iliajiri Watumishi wa Kada za Afya 10,328 na kati ya hao Halmashauri ya Mji Nanyamba ilipata Watumishi 51 wa kada mbalimbali za afya.

Dk. Dugange alisema Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa wataalam wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aidha, alisema Kituo cha Afya Majengo kilipangiwa watumishi nne ambao ni Mteknolojia Maabara, Tabibu Msaidizi na Wauguzi wawili.

Dk.Dugange alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imepeleka vifaa na vifaa tiba katika Halmashauri ya Nanyamba vyenye thamani ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya vituo vya huduma za afya.

About the author

mzalendoeditor