Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO ATOA SIKU 30 KWA NEMC KUONDOSHA MIFUKO YA PLASTIKI ISIYORUHUSIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano ulioufanya leo Aprili 6, 2023 Jijini Dodoma kuhusu tamko la serikali la katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Catherine Bwamenzaki na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bw. Menan Jangu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ametoa siku 30 kwa Mameneja wa Kanda zote wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuendesha kampeni za kuondosha mifuko ya plastiki isiyoruhusiwa kisheria inayochangia katika ongezeko la uchafuzi wa mazingira hususan maeneo ya mijini.

Akitoa tamko la Serikali kuhusu katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Aprili 6, 2023 Dkt. Jafo amesisitiza kuwa Meneja yoyote wa NEMC atayeshindwa kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo katika eneo lake atatakiwa kuachia ngazi moja na kuwaachia watendaji wenye uwezo wa kutimiza wajibu huo.

Dkt. Jafo amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kubebea bidhaa na matumizi ya mifuko isiyoruhusiwa kisheria, kinyume cha Kanuni ya 6 ya Kanuni za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019 na hivyo kuibua changamoto ya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya miji.

“Vifungashio hivyo, vinakosa sifa na hivyo kutokidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Hali hii inachangia katika ongezeko la uchafuzi wa mazingira hususan maeneo ya mijini na hali hii inaonesha ukiukwaji mkubwa wa Kanuni ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki unaofanywa na baadhi ya wazalishaji na wasambazaji” amesema Dkt. Jafo.

Waziri Jafo ameiasa jamii na kueleza kuwa makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio hivyo kuwa mifuko ya kubebea bidhaa, na kwa mujibu wa sheria, adhabu stahiki zitatolewa kwa wanaokiuka sheria wakiwemo watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa.

Aidha Dkt. Jafo amezitaka Sekretarieti za Mikoa, Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zote nchini kuendelea kudhibiti matumizi ya vifungashio visivyoruhusiwa kisheria kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ni jukumu la wadau wote.

Itakumbukuwa kuwa tarehe 1 Juni, 2019, Serikali ilipiga Marufuku uzalishaji, uingizaji nchini, usafirishaji nje ya nchi; usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kutumika kama vibebeo na vifungio katika bidhaa mbalimbali.

About the author

mzalendoeditor