Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa mkoa wa Simiyu wakati wa uzinduzi huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tatu kushoto) wakifungua pazia kuashiria uzinduzi wa tawi jipya la benki ya NBC Mkoa wa Simiyu wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi hilo iliyofanyika mkoani humo mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mbunge wa Bariadi na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (kushoto), viongozi wengine wa chama na serikali pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati) akikata utepe kuashiria na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa tatu kushoto) kuashiria uzinduzi wa tawi jipya la benki ya NBC Mkoa wa Simiyu wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi hilo iliyofanyika mkoani humo mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi ( kushoto) viongozi waandamizi wa chama na serikali pamoja na maofisa waandamizi wa benki hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (katikati) akielezea kuhusiana na huduma za benki hiyo tawi jipya la Simiyu wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa tawi hilo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa chama na serikali pamoja na maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wan ne kushoto) wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (Katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo wakati wa hafla hiyo.
We did it! Ndivyo wanavyoonekana kusema wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (katikati) ikiwa ni ishara ya kujipongeza kwa kufanikisha uzinduzi wa tawi la benki hiyo Mkoani Simiyu.
Muonekano wa tawi jipya la benki ya NBC Mkoa wa Simiyu.
Hafla hiyo ilipambwa na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya Sanaa kutoka mkoa wa Simiyu
Na.Mwandishi Wetu-SIMIYU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua tawi jipya la Benki ya NBC mkoa wa Simiyu huku akiipa changamoto benki hiyo kuhakikisha inafungua zaidi fursa za kiuchumi na uzalishaji mkoa huo hususani kupitia sekta za biashara, kilimo na ufugaji.
Akizungumza mara tu baada ya kuzindua tawi hilo jipya mkoani humo mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu Majaliwa aliekuwa ameambatana na viongozi waandamizi wa serikali na chama wa mkoa huo aliuomba uongozi wa benki hiyo kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele kuwasaidia wakazi wa mkoa huo kuondoakana na changamoto kubwa inayowakabili ya ukosefu wa mitaji.
“Mkurugenzi wa NBC pamoja na menejimenti yako mmefanya kazi nzuri sana kuleta huduma huduma zenu mkoani Simiyu. Huu ni mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa zao la pamba nchini huku pia wakazi wake wakijihusisha na shughuliza biashara na ufugaji. Ila kwa muda mrefu wakazi hawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Nimefurahi kusikia kwamba NBC mmekuja mkiwa na nia ya kumaliza changamoto hiyo nami nawasihi wana Simiyu benki hii iwe kimbilio lenu,’’ alisema.
Pamoja na changamoto ya ukosefu wa mitaji, Waziri Mkuu Majaliwa alibainisha kuwa wakazi hao wamekuwa wakikabiliwa na hofu ya kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukubwa wa riba. Alisema serikali tayari imekaa na taasisi za fedha nchini ikiwemo benki ya NBC ili kuona namna ya kupunguza riba hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa ujio wa benki hiyo mkoani humo umekuja wakati muafaka kwa kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ukuaji na uendeshaji wa biashara mkoani humo licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika maeneo mbalimbali ikiwemo uboreshwaji wa barabara kuu na kituo kikubwa cha mabasi ambacho kwasasa hakitumiki licha ya kugharimu fedha kiasi cha sh bilioni 7.
Awali akizungumzia tawi hilo jipya, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alisema hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa benki hiyo wa kutoa huduma zake katika mikoa yote ya Tanzania ili kuwafikia watanzania wengi zaidi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwajumuisha watanzania wengi zaidi kwenye mfumo rasmi wa fedha.
“Mkoa wa Simiyu ni kiungo muhimu sana katika uchumi wa kanda hii ya ziwa na taifa zima kwa ujumla. Hivyo uwepo wa mfumo rasmi wa kibenki, kupitia tawi hili la Benki ya NBC hapa Bariadi, utasaidia sana kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kufungua fursa mpya za kifedha. Hapo awali, wateja wetu walikuwa wakipta huduma kupitia mtandao wetu wa Wakala ambapo hapa Simiyu tuna zaidi ya mawakala 30.’’ alisema
Bw Sabi alibainisha kuwa benki hiyo ipo tayari kuhudumia makundi yote ya jamii ikiwemo taasisi za serikali, watumishi wa serikali, wafanyabiashara na wanafunzi.
“Sambamba na hilo, tawi hili pia linakusanya maduhuli serikali kupitia Mfumo wa Ukusanyaji wa Fedha za Umma (GePG) na kodi kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hivyo nawaomba sana wananchi wa mkoa wa Simiyu na maeneo ya Jirani kulitumia tawi vyema tawi hili ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi.’’ Alisema.
Ikiwa ni benki ya tatu kwa ukubwa nchini ikiwa inamiliki mali (Assets) zenye thamani ya TZS 1.52 trilioni na amana (Deposits) zenye thamani ya TZS 1.96 trilioni na wafanyakazi wapatao 977, benki ya NBC inajivunia mtandao mkubwa wa huduma unaojumuisha matawi 48, mashine za kutolea fedha (ATMS) 180, NBC Wakala zaidi ya elfu tisa huku ikiwa imewekeza zaidi huduma zake kupitia simu za mikononi “NBC Kiganjani” na Huduma za mtandao wa internet .