Featured Kitaifa

TANESCO YAPOKEA MASHINE UMBA YA KWANZA KATIKA KITUO CHA KUPOZA UMEME CHALINZE

Written by mzalendoeditor

Na. Mwandishi wetu-TANESCO

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mara ya kwanza limeanza kupokea moja ya mashine umba (Transforma) kubwa sita yenye uwezo wa megavoti 250 katika kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze  ambapo kati ya mashine umba hizi sita, mashine umba nne zitakuwa zikipokea umeme mkubwa wa kilovoti 400 utakaosafirishwa kutoka katika Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) na kuupoza hadi  kilovoti 220 na mashine umba mbili ni kwa ajili ya kuupoza umeme mkubwa kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 132.

Akiongea mara baada ya kupokea mashine umba (Transforma) hiyo Chalinze mkoani Pwani , Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, amesema kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze kitagharimu kiasi cha shilingi bilioni 128 na mpaka sasa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 53.13 na unatarajiwa kukamikia ifikapo tarehe 30 Julai 2023 ambapo kituo kitaweza kusafirisha hadi megawati 800 za umeme katika miundombinu ya umeme iliyopo sasa hivi. 

“Kituo hiki ambacho ndio kinapoza umeme kwa hapa Chalinze kitagharimu shilingi bilioni 128 na ujenzi wake umeshakamilika kwa asilimia 53.13. Leo tumepokea Transfoma kubwa kabisa,  ni transfoma ya kwanza  ambayo itafungwa hapa  kimsingi kituo hiki kitafungwa transfoma sita  na Reactors mbili  na vifaa vyote vimeshafika katika bandari yetu ya Dar Es Salaam. Matarajio yetu ni kwamba kituo hiki hadi kufikia  Julai 2023 mwaka huu  kitakuwa kimeshaanza kusafirisha hadi megawati  800  za umeme kupitia miundombinu ya umeme iliyopo, kwa hiyo haya ni mafanikio makubwa  watanzania lazima tujivunie  kwa sababu umeme ni uchumi, umeme ni uhai, umeme ni maisha na umeme ni maendeleo” amesema Mhe. Kunenge

Aidha Mhe. Kunenge ameeleza kuwa  mradi wa umeme wa bwawa la Julius Nyerere utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika hasa kwa Mkoa wa Pwani  ambao utasaidia sana katika kuendeleza ukuaji wa viwanda katika mkoa huo.

“Mkoa wa Pwani umeme kwetu ni jambo kubwa  kama ilivyo kwenye maeneo mengine, kwa hiyo kwa kituo hiki kufanya kazi maana yake ni kwamba  Bwawa la Julius Nyerere linazalisha umeme  wa kilovoti 400 ambao utasafirishwa na kupokelewa hapa na Transifoma hizi zitaupunguza mpaka kilovoti 220 na trasforma nyingine mbili zitauunguza umeme kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 132 ili uweze kutumika katika  Gridi yetu na katika mfumo wetu wa umeme maana yake ni kwamba inaleta ahueni  kwanza  kwa kupatikana umeme mwingi na wa uhakika na wamiliki viwanda wanahitaji umeme wa uhakika kwa hiyo nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuuendeleza Mradi huu wa Umeme” alishukuru Mhe. Kunenge.

Kwa upande wake Meneja miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Didas Lyamuya ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza na kujenga viwanda vingi Mkoani Pwani kwa sababu kukamilika kwa kituo hiki cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze kitawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika  katika mkoa huo lakini pia mikoa ya jirani kama Tanga, Arusha, Dodoma na Dar Es Salaam.

“Hiki kituo kinapokea umeme ambao unatoka Julius Nyerere na kufanya umeme wetu unaozalishwa Kinyerezi, Kihansi, Tegeta, Songasi na Ubungo kuja hapa na kuanza kusafirishwa, kwa hiyo wakazi wa Mkoa wa Tanga, Arusha, Dodoma na Dar Es Salaam  watanufaika na kituo hiki kwa sababu nyaya zetu na miundombinu yetu ilikuwa imetengana lakini sasa zote zitaanzia hapa, kwa hiyo wananchi  na wakazi wa hapa watakuwa na umeme wa kutosha kwa hiyo ni wakati mzuri sasa kwa wawekezaji kuweka viwanda kwa sababu tuna uhakika na umeme  wa kutosha” amesema Mhandisi Lyamuya.

Aidha, kituo hiki cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Chalinze chenye thamani ya shilingi bilioni 128 zinazogharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilianza kujengwa mnamo mwaka 2021 na mkandarasi TBEA kutoka China. Aidha, ujenzi wa kituo hiki umefikia asilimia 53.13 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2023.

About the author

mzalendoeditor