Featured Kitaifa

WAZIRI MHAGAMA AELEKEZA MIRADI YA TASAF YA AFYA NA ELIMU IKAMILIKE KWA WAKATI ILI ITOE MCHANGO KATIKA MAENDELEO YA TAIFA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa wa Jiwe Kuu na Mihama, Kata ya Kitangiri, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Sehemu ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na Wananchi wa Mtaa wa Jiwe Kuu na Mihama, Kata ya Kitangiri, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima wakifurahia jambo walipokuwa wakisikiliza taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilaya ya Ilemela  wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.

Mwonekano wa jengo la wodi ya wagonjwa wa nje (OPD) pamoja na huduma ya mama na mtoto, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza inayojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Mwanza alipowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamagana pamoja na Wananchi wa Kata ya Butimba wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF inayofadhiliwa na Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC) katika Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Sehemu ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamagana na wananchi wa Kata ya Butimba wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF inayofadhiliwa na Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC) katika Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Mwonekano wa jengo la bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyamagana linalojengwa na Serikali kupitia TASAF chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC) katika Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamagana, Zeana Deus akiishukuru Serikali kupitia TASAF kwa kujenga madarasa na mabweni shuleni hapo yatakayowasaidia kupata elimu bora ili watimize malengo yao.

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewaelekeza viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza kusimamia ukamilishaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ya afya na elimu ili itoe michango katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.

Mhe. Jenista amesema hukuna sababu ya kusuasua katika ukamilishaji wa miradi hiyo ya afya na elimu kwa kuwa ni miradi muhimu sana na ikizingatiwa kuwa fedha yote ya ujenzi wa miradi hiyo ilishatengwa na kutolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhe. Jenista amesisitiza usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya afya na elimu ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF ametoa fedha nyingi ili iwanufaishe walengwa na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hizo muhimu kwa jamii.

Mhe. Jenista amesema miradi yote ya elimu inayotekelezwa na TASAF itasaidia sana kuandaa rasilimaliwatu itakayoendeleza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta maendeleo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Shule hizi zinazojengwa kama zitatoa elimu bora kwa wanafunzi na wakapata ufaulu mzuri, nina hakika watakuwa ndio madaktari, walimu, wahandisi, wabunge, wakuu wa wilaya na viongozi wa vyama vya siasa wajao na kuongeza kuwa TASAF inandaa rasilimaliwatu ya kesho itakayokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Akizungumzia faida ya miradi ya afya inayotekelezwa na TASAF, Mhe. Jenista amesema miradi hiyo ikikamilika itatoa huduma bora za afya kwa watumishi wa umma na wananchi ili waweze kuwa na afya bora inayowawezesha kushiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

“Tukiwa na afya njema, tutashiriki vizuri shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye utekelezaji wa miradi ya afya ya TASAF utakuwa umechangia katika maendeleo ya taifa letu,” Mhe. Jenista amefafanua.

Kwa upande wake, mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamagana, Bi. Rachel Juma amesema, wanafunzi wa shule hiyo wanaahidi kutomuangusha Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusoma kwa bidii ili kuunga mkono jitihada zake za kuboresha mazingira ya shule yao kupitia fedha za TASAF.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo ya Nyamagana, Bi. Zeana Deus amesema kuwa, atayatumia vema madarasa yaliyojengwa na TASAF ili kutimiza ndoto yake ya kufanya vizuri katika masomo ya sayansi kwa ajili ya maisha yake ya baadae na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Naye Bw. Shaban Jafari ambaye pia ni mwanafunzi wa shule hiyo ya Sekondari Nyamagana amesema kuwa, awali kabla ya TASAF kujenga madarasa katika shule yao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa, hivyo wanamshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwajengea madarasa kupitia TASAF.

Sanjari na hao, Mkazi na Mlengwa wa TASAF wa Wilaya ya Nyamagana Bi. Ratifa Zanziba ameishukuru TASAF kwa kujenga madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari ya Nyamagana ambapo imewaondolea adha wanafunzi kulazimika kwenda umbali mrefu kuitafuta elimu.

Mkazi mwingine ambaye pia ni mlengwa wa TASAF Wilaya ya Nyamagana Bi. Ziada Basil ameungana na mwenzie kuishukuru TASAF kwa kujenga madarasa na zahanati katika wilaya yao ili kuwahudumia wananchi wa eneo hilo.

TASAF imeendelea kugusa maisha ya wananchi katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza kupitia utekelezaji wa miradi yake ya Afya na Elimu ambayo inafadhiliwa na Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC).

About the author

mzalendoeditor