Featured Kitaifa

PROF. MAKUBI APONGEZA KITENGO CHA HABARI KWA KAZI NZURI

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi pamoja na Menejimenti wamepongeza Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU) kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu taarifa mbalimbali za sekta ya afya.

Prof. Makubi ametoa pongezi hizo leo mara baada ya kukabidhiwa Tuzo ya Kutoa Taarifa za Serikali kwa Umma ya mwaka 2022 ambapo iliibuka mshindi wa kwanza kati ya Wizara 10 zilizochaguliwa kushindanishwa.

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw. Aminiel Aligaesha katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.

Pamoja na juhudi zilizosababisha Wizara ya Afya kuwa mshindi wa kwanza kwa kutoa taarifa kwa umma Prof. Makubi ametaka kitengo hicho kuongeza kasi ya kuhabarisha wananchi kwakuwa Wizara ina mambo mengi ambayo wananchi wanapaswa kuyafahamu.

Tuzo hii ni ya pili kwa mwaka huu kwa Wizara ya Afya kupitia kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupata tuzo ambapo baada ya Mwezi Februari 2022 kupata tuzo ya mshindi wa kwanza upande wa Wizara kutoka Tanzania Digital Award iliyotambua mchango wa Wizara kuhabarisha umma kupitia mitandao ya kijamii.

About the author

mzalendoeditor