Na Ndahani Lugunya,Kongwa.

Mratibu wa Idara ya Elimu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Padri Chrisant Mganga,amewaomba Viongozi wa Serikali na wa Kijamii katika Mataifa ya kiafrika,kutokukubali kuruhusu vitendo vinavyopingana na mpango wa uumbaji wa Mungu ikiwemo Ushoga na Usagaji kwa kisingizo cha haki za Binadamu.

Amesema hayo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye Mahafali ya 7 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mt.Crala iliyopo Parokia ya Mt.Theresia wa Mtoto Yesu-Mlali,Dekania ya Mt Fransisko wa Asisi-Kongwa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

Padri Mganga amesema kwamba kwa bahati mbaya kwa sasa wapo baadhi ya Viongozi katika nchi za Kiafrika wamerubuniwa na kuruhusu vitendo vya ushoga na usagaji katika Matifa yao,kwa sharti la misaada wanayopokea kutoka katika mataifa hayo ambayo yamehalalisha vitendo hivyo.

“Tunawaomba Viongozi wetu wawe na hofu ya Mungu.kuna mambo ya ushoga ambayo yanaendelea mitaani na kwenye taasisi zetu tunajifanya kama hayapo hivi lakini yapo yanatumomonyoa na yanatumaliza.

Usagaji upo hatutaki kusema lakini yapo yanaendelea kwa siri na nimitandao kuna watu wanaofanya hayo kwa kigezo cha haki za binadamu wanatengeneza mitandao na watoto wetu wanaingia humo.Wakatoliki  tuwe makini katika taasisi zetu tusiwe na maskendo kama hayo.

Nawaomba kila mmoja ajitambue katika nafasi yake tuondokane na maskendo ambayo yanatuaibisha katika Taifa,Serikali,Kanisa na katika jamii kwa ujumla.kila mmoja mmoja achukue hatua ya kuangalia tunavyoenenda na tujitahidi kuwa na hofu ya Mungu,” amesema Padri Mganga.

Amesema kamwe Wakristo Wakatoliki na watu wote wenye mapenzi mema wasiyape nafasi mambo yanayoharibu utamaduni na maadili ya kiafrika,lakini kubwa zaidi mambo hayo yanapingana na mpango wa uumbaji na uadilifu wa Mwenyezi  Mungu.

“Wanatumia kivuli cha nyota za kijani na haki za binadamu kutimiza azima yao na pasipo kujua watu wetu wananaswa na mambo hayo.Kanisa Katoliki linakataa kuhusu matumizi ya vidonge na vipandikizi vya kuzuia mimba lakini watu wanachangamkia na hayo ndiyo yanawaharibu na wengine wanatetea kabisa kwamba hii ni haki yangu,” amesema. 

Hata hivyo amewaomba Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwaombea Viongozi wa Serikali ili wasichukue kila kitu kutoka katika Mataifa ya nje kwa kisingizio cha haki za Binadamu,ambapo matokeo yake ni kuharibika kwa jamii na hapatakuwa na njia ya kutoka katika janga hilo.

“Tujitahidi kuwa na hofu ya Mungu.Viongozi wetu tuwaombee wa Serikali ili wasichukue kila kitu kutoka huko nje kwa kisingizio cha haki za binadamu halafu jamii yetu inaharibika tukabaki kila mmoja analalamika hatujui cha kufanya,” Amesema Padri Mganga.

Hata hivyo Padri Mganga ameongeza kuwa vitendo viovu vinavyotokea katika jamii ya sasa ni kwa sababu ya uzembe wa malezi na maadili.

“Yanayoendelea sasa hivi ukisikia Baba kazaa na mtoto wake wa kumzaa.Mama ameolewa na mtoto wake.mtawa amevunja ndoa ya mtu au Padri amefanya mambo ya ajabu kwa watoto ni kwa sababu ya uzembe wa malezi na maadili.

Kwahiyo lazima tuambiane ukweli na tuyafanyie kazi kamwe tusibweteke na kuendelea kufurahi na kuambiana maneno matamu haya mengine ambayo yanatumaliza tunanyamazia.naomba tuyaongelee na tuyafanyie kazi  ili jamii iweze kubadilika kuanzia kwenye familia taasisi zetu na jamii nzima ya watanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa Wakristo Wakatoliki kujitahidi kukwepa mafundisho ya Injili ya mafaniko  yanayohubiriwa kila kukicha.

Amesema kwa sasa kumeibuka utitiri wa Makanisa na wahubiri wa kila aina wanaojivisha vyeo na kutangazia watu Injili ya mafanikio,na kufanya kundi kubwa la watu kukimbilia mafundisho hayo jambo linakwenda kinyume na mafundisho ya Kristo Yesu.

“Kuna kitu kinaitwa Injili ya mafanikio.sasa hivi  kuna madhehebu yanaibuka kila mahali watu wanaanzisha makanisa na wanajipa na vyeo.kwa sasa hadi wasanii wa nyimbo za kidunia wengine wamekuwa na makanisa yao na tunawafahamu.watu wanatafuta namna ya kuishi.

Kwa hiyo makanisa yanatangaza Injili ya mafanikio yaani kama ni mwanafunzi unaambiwa hata usipo soma wewe siku ya mtihani utafanya vizuri na utafaulu.wapo pia wanaodanganywa kwamba kama hujaolewa na ukienda kusali kwao kuna upepo wa kisulisuli utapa mume.

Kama ulikuwa umetoa mimba kizazi kikaharibika ukienda kusali kwao au ukiwe kwenye runinga unaambiwa nakuombea shika hapo panapouma kama ni kwenye kizazi shika hapo mimi nakuombea na baada ya kuombewa hapo hapo unapona na kizazi kinarudi.tambua kwamba ukishaharibu kizazi  hakiwezi kurudi na hakuwezi kutokea muujiza hapo,” amesema Padri Mganga.

Kutokana na hilo Padri Mganga amewataka Vijana kukwepa mafundisho ya namna hiyo yanayoweza kuja kuwaletea madhara badae,huku akiwahimiza kufauta mafundisho sahihi wanayofundishwa.

“Mtalia miaka yote juu ya vidonda vya tumbo kwa sababu ya kwenda kudanganywa huko.msiende jitahidini kukwepa Injili za mafanikio.unambiwa kama hauna gari ukienda kusali unapewa.kuna vitambaa vya upako na mafuta ya upako na mkienda huko mnapewa hayo mafuta na vitambaa.tujitahidi kukwepa vile ambavyo vinatuharibu imani yetu na tujitahidi kufuata yale ambayo ni ya msingi tunayofundishwa,” amesisitiza Padri Mganga.

Amewataka Wakatoliki na Wakristo wote kwa ujumla kuchuja mafundisho sahihi yanayotolewa na wahubiri wa sasa wanaozuka kila kukicha,kwani wengi wao wapo kimaslahi na si kwa ajili ya kuongoa roho za watu,huku akikazia suala la malezi adilifu kwa vijana mintarafu mafundisho ya Kanisa.

Previous articleWAZIRI DKT. GWAJIMA: WARAKA WA VIBOKO SHULENI USAMBAZWE
Next articleWIZARA YA VIWANDA YATOA AGIZO KWA MAOFISA BIASHARA NCHI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here