Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuusambaza waraka wa adhabu za viboko shuleni wa mwaka 2002 ili walimu na wanafunzi wauelewe.

Waziri Gwajima amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya haki za watoto yaliyofanyika jijini Dar es salaam Novemba 29, 2022.

Amesema ukatili kwa watoto unaendana na kuudhuru mwili ikiwa ni pamoja na vipigo ikijumuisha adhabu ya viboko vilivyopitiliza mashuleni.

“Hivyo viboko vilivyopitiliza ni ukatili kwa watoto kwakuwa tunao Waraka na 24 wa mwaka 2002 unaosimamia adhabu za viboko mashuleni ambao unasema wazi ni nani mwenye Mamlaka yakutoa adhabu hiyo na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi. Najua changamoto iliyopo ni usimamizi wa utekelezaji wa Waraka huo, baadhi ya Walimu hawaufuati wanapotoa adhabu, hawa walimu nawataka wabadilike vinginevyo sitamwaacha mwalimu asishtakiwe kwa sheria ya mtoto iwapo atatoa adhabu hiyo nje ya Waraka huo, sitamwacha” amesema Waziri Gwajima.

Aidha amewahakikishia watoto kwamba timu ya Serikali, wadau na jamii watakutana kuona namna nzuri ya kulishughulikia hoja ya viboko kwa kuzingatia maadili na tamaduni katika malezi.

“Inasikitisha kuona baadhi ya watoto wanaacha shule kwa sababu ya kukimbia viboko huku wengine wakipata majeraha makubwa na ulemavu na hata kupoteza maisha eti kwa sababu ya adhabu za viboko, hii haikubaliki kwani hii adhabu ya viboko haikulenga kusababisha mateso kwa watoto na ndiyo maana tunao Waraka”

Ameongeza kuwa Serikali itaziimarisha Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawke na Madawati ya Ulinzi wa Watoto Mashuleni ili waufahamu Waraka wa Viboko waujue wasifanyiwe kinyume na wakibaini kuwa ni kinyume wapaze sauti haraka.

Waziri Dkt. Gwajima pia amewaonya wanaume wanaobaka na kulawiti watoto kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo hivyo na sheria itaendelea kuchukuliwa kwa wote watakaobainika.

Awali, watoto walioshiriki maadhimisho hayo wameeleza baadhi ya hoja zao kwa Waziri ikiwemo kuomba marekebisho ya sheria ya ndoa, kupata huduma na taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi pamoja na kuondolewa kwa adhabu zinazodhuru mwili hasa viboko.

Kwa upande wa viongozi wa Dini waiowakilishwa naKatibu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWAT) Shekh Nurdin wamesema wanashirikiana na Serikali katika kutoa maoni ya kurekebisha sheria ya ndoa ili kuwalinda watoto wa kike na ndoa za mapema.

Naye mwakilishi mkaazi wa shirika la watoto UNICEF Shalini Bahuguna ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kupunguza vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano na kusema kwamba Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutekeleza programu za watoto.

Previous articlePATA HABARI MOTO MOTO KATIKA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 30,2022
Next articlePADRI MGANGA:”MISAADA YA WAHISANI ISIWE CHANZO CHA KURUHUSU VITENDO VYA USHOGA NA USAGAJI, AWATAHADHARISHA WAKRISTO JUU YA INJILI ZA MAFANIKIO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here