Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia  Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Mamlaka  za Bima Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha.  (AICC) 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha  (AICC) kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Mamlaka za Bima  wa  Afrika

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa  wa Wakuu wa Mamlaka za Bima Afrika wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia Mkutano huo kwenye Kituo cha Kimtaifa cha Mkutano cha Arusha (AICC)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia  Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Mamlaka  za Bima Afrrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha.  (AICC) 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Fedha Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba baada ya kuhutubia Mkutano wa Kimataifa wa  Wakuu wa  Mamlaka  za Bima Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Novemba 30, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

.……………………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka na taasisi zinazohusika na usimamizi wa bima na hifadhi ya jamii barani Afrika zitoe elimu ya kutosha kwa jamii ili watu wengi wajiunge na huduma hizo.

“Mamlaka na taasisi zetu zinazohusika na usimamizi wa bima na hifadhi ya jamii ongezeni juhudi ya utoaji wa elimu ya bima na hifadhi ya jamii barani Afrika kwa namna ile ambayo nchi husika itaona inafaa,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Novemba 30, 2022) wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Mamlaka za Bima barani Afrika ulioanza leo kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha. Mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali Afrika, unatarajiwa kumalizika Desemba 2, 2022.

“Takwimu zinaonyesha kwamba wastani wa uelewa kuhusu matumizi ya bima kwa watu wengi barani Afrika bado ni mdogo. Hivyo basi, tutumie vema fursa ya uwepo wa mkutano huu kuongeza juhudi na tuje na mikakati itakayohakikisha watu wetu wanapata elimu hii muhimu,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Akifafanua kuhusu makubaliano ya kuwa na eneo huru la biashara kwa bara la Afrika (yaani African Continental Free Trade Area), Waziri Mkuu amesema utiaji saini wa utekelezaji wa makubaliano hayo ulifanyika Januari mosi, 2021 na sekretariati yake ipo Accra, Ghana.

“Makubaliano ya Eneo Huru la Biashara ya Bara la Afrika yanalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika. Makubaliano haya yameleta pamoja nchi 54 za Afrika na kuunda soko moja la watu takribani bilioni 1.4.”

“Wataalamu wanakadiria kwamba iwapo tutaendeleza ushirikiano huu kwa kufanya biashara huru miongoni mwetu, bila shaka  pato la Bara la Afrika litakua kwa wastani wa asilimia 6 hadi kufikia takriban dola trilioni 66.4 kwa miaka 50 ijayo,” amesema.

Amesema Bara la Afrika lina rasilmali nyingi zikiwemo ardhi ya kilimo, mafuta, misitu, madini, mifugo na kwamba lina rasilmaliwatu ya wakazi bilioni 1.4 ambayo ni sawa na asilimia 18.2 ya watu wote duniani. “Hii ni fursa kubwa ambayo inapaswa kujadiliwa kwa undani na kuwekewa mikakati kwenye mkutano huu. Ninaomba nitoe rai kwamba mkutano huu ujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuzifikia na kuzitumia fursa zilizopo kwenye eneo huru la biashara ya Barani Afrika kwa ajili ya maendeleo ya bara la Afrika na watu wake,” amesisitiza.

Akielezea kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, Waziri Mkuu amesema ni vigumu sana kutenganisha umuhimu wa bima na hifadhi ya jamii kwa sababu vyote vinajaribu kumlinda mtu na jamii dhidi ya majanga yanayoweza kutokea wakati wowote.

Amewataka wataalamu hao waangalie namna ya kuifanya mifumo ya hifadhi ya jamii na pensheni iwe shirikishi kwa watu wote  na hasa kuwapa kipaumbele wanawake, vijana, wazee na wakulima ambao wako katika mazingira magumu.

“Hapa Tanzania,  Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa kipaumbele kwenye suala la kuwezesha jamii kwa kuwainua kiuchumi wanawake na vijana ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Ouagadougou (“Ouagadougou+10”) la Utekelezaji wa Mpango wa Ajira na kutokomeza umaskini ambalo lilipitishwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika Januari 2015 kama Ajenda ya AU ya 2063.

“Ni wakati muafaka mifuko yetu ya jamii kusaidiana na Serikali zetu kuondoa umasikini miongoni mwa watu wetu. Nitoe rai kwa washiriki wa mkutano huu muangalie  uwezekano wa kujadili kwa mapana kuhusiana na namna ya mifuko ya hifadhi ya jamii inavyoweza kusaidia kuinua uchumi wa watu wetu na kusaidia kuondoa umaskini hasa kwa wanawake, vijana na wakulima.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema eneo la bima lilishatolewa maelekezo na Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 22, 2021 wakati alipohutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

“Mheshimiwa Rais alielekeza kwamba suala la bima ya kilimo na bima ya afya kwa wote liangaliwe kwa ukaribu zaidi na kuwekewa mfumo mzuri wa kisheria utakaoainisha namna bora ya utekelezaji wake.”

Alisema Serikali iliangalia pia suala la ukingaji wa majanga kwenye maeneo ya mikusanyiko kama vile masoko, shule na maduka na ikaamua kuweka mfumo wa kisheria wa namna ya kuyakinga majanga haya kwa njia ya bima kwa kupitisha Sheria ya Fedha Na. 05 ya Mwaka 2022 itakayosaidia kukinga maeneo yenye mikusanyiko kama vile masoko, vivuko na majengo ya biashara.

“Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania tunaandaa mwongozo wa bima ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha kundi hili kubwa linapata uhakika wa uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi hasa kwenye kipindi hiki chenye changamoto kubwa za mabadiliko ya tabia nchi.”

Previous articleWANAFUNZI WATAHADHARISHWA MATUMIZI MITANDAO YA KIJAMII, WATAKIWA KUTOTOA ‘PASSWORD’ ZA SIMU ZAO NA WAPENZI WAO
Next articleRAIS SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here