Featured Kitaifa

MAAFISA TARAFA NA WATENDAJI WA KATA WATAKIWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI WA MAPATO YA NDANI

Written by mzalendo

OR – TAMISEMI

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amewataka maafisa tarafa na watendaji wa kata kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi yake kwakuwa Serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.

Ameyasema hayo Aprili 23, 2024 wakati wa akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji wa kata wa mkoa wa Kagera yaliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Bukoba sekondari.

Mhe. Mwassa amesema Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya kazi kwa ubunifu na waledi lakini kuwataka kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na matumizi yake kwa kushirikiana na viongozi wa wananchi na watendaji wengine walipo katika maeneo yao ya kazi waliopo ngazi ya msingi.

“bila ushirikiano hakuna mafanikio ” Mhe. Mwassa amesema

Pia amewasisitiza maafisa hao kufuatilia na kusimamia vizuri fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoletwa na Serikali katika maeneo yao ili fedha hizo zilete matokea tarajiwa na kuwaondolea wananchi changamoto za kukosa huduma.

“Nyie ndio mpo katika kazi za msingi mnapaswa kufahamu na kuzingatia kanuni na maadili na kutumia misingi ya haki badala ya upendeleo pale mnapotoa huduma kwa wananchi na kuweka vizuri malengo halisi ya kazi zenu ili kuwawezesha kufikia kiwango cha juu katika utendaji wenu wa kazi kwa kuwatendea haki wananchi katika utoaji wa huduma” amesema Mhe. Mwassa.

Aidha, Mhe. Mwassa amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa akwta kuhakikisha wanasimamia usalama, amani na utulivu vinakuwepo kwenye maeneo yao wakati wote ikizingatiwa suala la usalama ni jukumu la kila mwananchi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama katika maeneo yao

“Kero ndogo ndio uzaa kubwa kwahiyo tujitahidi sana kutatua hizi kero ndogo ndogo ili tusije kutengeneza vinyongo na chuki kwa wananchi na Serikali yao”

Mhe.Mwassa amewakumbusha maafisa tarafa na watendeji wa kata kujipanga na kusimamia vizuri zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhakikisha kunakuwa na uhuru, haki na wananchi kushiriki.

About the author

mzalendo