Featured Kitaifa

MTATURU ANUSA HARUFU YA UPIGAJI NTUNTU

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa kituo cha afya cha Ntuntu kilichopo wilaya ya Ikungi Mkoani Singida ambacho hakijakamilika huku fedha zilizopelekwa zikiwa zimeisha.

Kutokana na hilo ametoa maombi matatu kwa serikali ikiwemo kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Angellah Kairuki kufika kutupia jicho kituo hicho.

Aidha,amemuomba Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kumtoa msimamizi wa mradi huo kutokana na kushindwa kutekeleza kazi aliyokabidhiwa.

Akizungumza Novemba 21,2022,baada ya kukagua kituo hicho ambacho kwa sasa ujenzi wake umesimama,Mtaturu ameishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),kufika ili kuchunguza mwenendo mzima wa ujenzi ulivyokuwa.

Mtaturu alisema April mwaka huu serikali ilipeleka Sh Milioni 250 kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi ambayo ilianza Juni mwaka huu na ilitakiwa ukamilike Octoba Mwaka huu lakini haukukamilika na kiasi cha fedha kilichopelekwa kiliisha.

“Huyu msimamizi wa mradi yeye mwenyewe anasimamia na yeye mwenyewe amejipa tenda hapa unategemea hizo fedha zisiliwe kwa kweli kwa maana ya utaratibu huyu msimamizi amekosa sifa, amempa tenda mke wake ya kusambaza vifaa,hatuwezi kukubali,hatusemi watu wasipewe tenda lakini wewe kama ni sehemu ya maslahi huwezi simamia mradi vizuri,

“Nimuombe DC,niwaombe TAKUKURU mje hapa,haiwezekani kiasi hicho hicho cha fedha kimepelekwa kituo cha Iglasoni Jimbo la Singida Magharibi kimekamilisha ujenzi ilhali kule miundombinu yake sio rafiki,barabara sio nzuri,mchanga hakuna maeneo ya jirani tofauti na eneo hili,”amesisitiza.

Amesema kilichotokea ni ubabaishaji wa kutoshirikisha kamati ya ujenzi katika mchakato mzima jambo ambalo limeleta sintofahamu kwa wananchi.

“Wananchi wenzangu nimekuja kuwahakikishia ,yoyote aliyechezea fedha za mama Samia hatabaki salama,mbunge nitasema hapa nitaenda kupiga kelele mpaka bungeni kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana,tunataka wananchi wa Ntuntu wapate huduma kama alivyolenga Rais wetu,wananchi kuweni na amani,wanasema chelewa ufike maadam tumegundua tatizo mapema naomba niwahakikishie kilio hiki nimefikisha kwa wakubwa,”amesema.

Ameongeza,“Mimi mbunge wenu nilienda bungeni kuomba fedha kwa ajili ya kituo hiki,na namshukuru Mh Rais alisikia kilio chetu akaleta Milioni 500 hapa ili kupunguza tatizo la kutembea umbali mrefu kufuata huduma, tulijua kituo kikijengwa hapa watu wa Misughaa,Mang’onyi,Lighwa wapo jirani watakuja kupata huduma badala ya kutembea kwenda Makiungu,lakini dhamira hii imekwamishwa na watu wachache,”amebainisha.

Mtaturu amesema kama viongozi hawawezi kuruhusu watu wachache warudishe nyuma juhudi za Rais Samia,“Tunampongeza na kumshukuru Rais wetu kwa kazi kubwa anayotufanyia,kumpongeza mtu ni kumtia moyo.

About the author

mzalendoeditor