Featured Kitaifa

TANZANIA MWENYEJI KONGAMANO LA 10 LA JOTOARDHI MWAKA 2024

Written by mzalendoeditor

Kamishna Msaidizi wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati Mha. Innocent Luoga akitoa taarifa ya Tanzania kukubali kuwa Mwenyeji wa Kongamano la 10 la Jotoardhi kwa Nchi za Ukanda wa Afrika lililofanyika tarehe 3 hadi  5 Novemba, 2022 katika Mji wa Heron, nchini Djibouti. 

Kamishna Msaidizi wa Umeme na Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati, Mha.Innocent Luoga, akizungumza wakati wa Kongamano la 10 la Jotoardhi kwa Nchi za Ukanda wa Afrika lililofanyika tarehe 3 hadi 5 Novemba, 2022 katika Mji wa Heron, nchini Djibouti. 

Ujumbe wa Tanzania uliohudhuria Kongamano la 9 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lililofanyika katika Mji wa Heron nchini Djibouti. Kutoka kushoto ni Mha Kato Kabaka (Mjumbe wa Kamati ya ARGeo), Mha.Mathew Mwangomba (Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC), Mha Innocent Luoga (Kamishna Msaidizi wa Umeme), Prof. Shubi Kaijage (Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC) na Mha.Shakiru Idrisa ( Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TGDC). 

…………………………………………………..

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la 10 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Mashariki ya Afrika (African Rift Geothermal Conference – ARGeo) litakakofanyika Mwaka 2024.

Hayo yameelezwa katika Kongamano la 9 la Jotoardhi la Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lililofanyika katika Mji wa Heron nchini Djibouti ambalo lilijadili uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi katika kuzalisha umeme na matumizi mengine.

Akimwakilisha Waziri wa Nishati kwenye Kongamano hilo, Kamishna Msaidizi wa Umeme Mha. Innocent Luoga alisema “tupo tayari kuwa wenyeji wa Kongamano la 10 la Jotoardhi litakalofanyika Mwaka 2024 ili tuweze kupata manufaa ya kongamano hilo ikiwa pamoja na kuharakisha kupata umeme  unaotokana na Jotoardhi.”

Mhandisi  Luoga alieleza kuwa, pamoja na kuimarisha ushirikiano na nchi wanachama, Tanzania itanufaika na kongamano hilo kwa kuhamasisha uendelezaji wa Jotoardhi nchini, kupata fedha za kutekeleza Miradi ya Jotoardhi, pamoja na kubadilishana uzoefu na nchi zilizofanikiwa katika kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi zikiwemo Kenya na Ethiopia. 

Katika Kongamano hilo, Wizara ya Nishati pamoja na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) zilipata fursa za kufanya vikao na Mashirika mbalimbali yanayofadhili Miradi ya Jotoardhi ili kupata fedha za kutekeleza Miradi hiyo. Mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Mfuko wa Kuzuia Athari za Jotoardhi (GRMF) na Benki ya Maendeleo ya Biashara ya Afrika (TDB).

Kamishna Luoga aliambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi nchini (TGDC) Prof. Shubi Kaijage, Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC, Mha. Mathew Mwangomba, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TGDC Mha. Shakiru Kajugus pamoja na Mjumbe wa Kamati ya ARGeo Mha. Kato Kabaka.

About the author

mzalendoeditor