Featured Kitaifa

NIT YANUNUA NDEGE  MBILI KUANZA KUTUMIKA KUFUNDISHA MARUBANI NDANI YA NCHI

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof. Zakaria Mganilwa,akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimenunua ndege mbili ambazo zitaanza kutumika kufundisha Marubani ndani ya nchi ili kupunguza gharama za masomo ya fani hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkuu  wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof. Zakaria Mganilwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

Prof.Mganilwa ameeleza  lengo la kununuliwa kwa ndege hizo mbili ni kukiwezesha chuo hicho kuanza kutoa mafunzo ya Urubani nchini.

“Ndege hizi mbili za injini moja zitakuwa zinatumika kwa ajili ya kujifunza lakini pia badae zitanunuliwa nyingine mbili za njini mbili kwani ni lazima rubani aendeshe ndege ya injini moja na baadae injini mbili ili aweze kuajiriwa na mashirika ya ndege”amesema Prof. Mganilwa

Hata hivyo amesema kutokana na chuo hicho kuanza kutoa mafunzo ya Urubani nchini kutasaidia kupunguza gharama kubwa za kusomesha watu nje ya nchi.

“Kumfundisha Rubani mmoja nje ya nchi ni Shilingi milioni 200, hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya Shirika la Ndege Nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu Wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini,
Na kuongeza “Hivi sasa tuna ndege 400 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya Marubani ni wageni, hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea Urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi na Kwa uwekezaji huu unaofanyika, tuna matumaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania litaweza kuwa Shirika bora kwa Afrika,” Prof.Mganilwa

Prof. Mganilwa amesema chuo hicho pia kimeanza kutoa kozi ya ufundi wa kutengeza na kusanifu Meli ili kuepuka changamoto iliyowahi kujitokeza hapo awali ya kufa kwa shirika la Meli nchini.

“Hivi sasa vijana wapo katika mafunzo ya kutengeneza meli pamoja na usanifu wa meli na hii inamaanisha kuwa hadi mwakani tutakuwa na vija wengi waliohitimu mafunzo na wenye ujuzi huu ambao watatumika kutoa huduma katika mashirika ya Meli nchini”amesema

Aidha amesema kuwa Serikali imekopa takriban Sh49 bilioni kutoka kwa Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga na Operesheni za Usafirishaji ambacho kina majukumu ya kutayarisha wataalam wa sekta ya usafiri wa anga.

“Fedha hii imegawanywa katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia Wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar es Salaam kwa gharama ya Sh21 bilioni na baadae tutajenga majengo mkoani Kilimanjaro kwa sababu lazima marubani wafundishiwe ndani ya viwanja vya ndege,”amesema.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa,amesema kutokana na serikali kuwekeza katika miradi mkubwa ya kimkakati chuo hicho kitakuwa msaada mkubwa katika uzalishaji wa rasilimali watu.

“Safari inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi itategemea sana kuwa na wataalam wetu wa ndani kwani hatuwezi kunufaika na thamani ya miradi yetu kama tunategemea wataalam kutoka nje,”Amesema Msigwa

Bw.Msigwa amesema kuwa NIT itawezesha vijana wetu kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalan ndege tano zinazotarajiwa kuja nchini, ambapo kwa mwaka 2023, ndege nne zitaingia nchini.

MKUU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof. Zakaria Mganilwa,akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

MKUU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof. Zakaria Mganilwa,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa,akizungumzia na waandishi na habari (hawapo pichani) kuhusu mazuri yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita mara baada ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)  kutoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor