Featured Kitaifa

WAZIRI GWAJIMA AWATWIKA WAZEE JUKUMU LA MALEZI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wazee wanaume waliohudhuria hafla ya Harambee ya kukiimarisha Chama cha Wazee Wanaume Tanzania iliyofanyika jijini Arusha.

………………….

Na WMJJWM-Arusha
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wanaume wazee  kuwaandaa na kuwalea vijana kwa ajili ya  maisha ya uzeeni.
Waziri Dkt. Gwajima ametoa rai hiyo wakati wa Uzinduzi wa harambee ya kuchangia chama cha Wanaume Wazee Tanzania kwa lengo la kukijenga na kukiimarisha iliyofanyika Jijini Arusha.
Amesema kutokana na mmomonyoko wa maadili ulioshamiri kwa sasa Wazee hasa wanaume wana nafasi kubwa wakiwa ni viongozi wa familia kukemea vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii ya kitanzania.
“Sasa hivi tunapita kwenye kipindi cha mmomonyoko wa maadili, kwani umeenea ndani ya jamii nyingi, ni changamoto sana na sisi kama Wazee tusiposimama vizuri kwa nafasi yetu kubeba ulezi wa jamii tunaweza tukajikuta tunapata Wazee wa kesho na keshokutwa ambao watashindwa kulea vizazi vinavyokuja” alisema Dkt. Gwajima.
Ameongeza kwamba, chombo hicho kina ulazima wa kuwa na jukumu la kujua kinafanya nini ili maadili ya vijana yaendelee kuwa mazuri kwa manufaa ya kizazi kijacho.
“Katika zama hizi tunahitaji zaidi Wazee waendelee kufanya mengi ili kuambukiza vizazi vipya tabia njema na kuwezesha nao kufikia uzee ulio mwema lakini cha kusikitisha hivi karibuni kumekuwa na Wazee wanaoripotiwa kufanya matukio ya ajabu yasiyolingana na umri wao mfano kubaka na kulawiti watoto, kuwaoza watoto wadogo na kupandikiza imani mbaya” aliongeza Dkt. Gwajima.
Gwajima amekitaka Chama hicho cha Wazee wanaume kushirikiana kwa karibu na Baraza la Ushauri la Wazee pamoja na Serikali katika kutekeleza afua mbalimbali kwa ustawi wa Wazee nchini.
Wakati wa hafla hiyo Dkt. Gwajima amebainisha juhudu za Serikali zinazofanywa kuhakikisha Ustawi wa Wazee ikiwemo kuimarisha mifumo ili wazee wapate huduma za kijamii kama Afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee, kupitia upya Sera ya Wazee na kuanzisha mabaraza ya wazee.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Chama cha Wanaume Tanzania Tadey Mchena amesema Chama kinakusudia kupata kiasi cha shilingi milioni 100 kwa lengo la kununua kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Chama, kuelimisha jamii, kuwasaidia wazee bima ya Afya na vitendea kazi.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama hicho John Sagata amesema Chama hicho kina malengo ya kuwasaidia Wazee katika masuala mbalimbali ikiwemo matibabu kupitia bima ya Afya, 
Wakati wa  harambee hiyo jumla ya Shilingi Millioni 30 kimepatikana ambapo ahadi ni Shillingi Millioni 11 na fedha tasilimu zilizotolewa ni Shillingi Milllioni 19 ikiwemo Shillingi Millioni 2  mchango wa Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wazee wanaume waliohudhuria hafla ya Harambee ya kukiimarisha Chama cha Wazee Wanaume Tanzania iliyofanyika jijini Arusha.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akimkabidhi Kiongozi Mkuu wa Chama cha Wanume Tanzania mchango wa Wizara Sh. Millioni mbili (2) kwajili ya kukiimarisha chama hicho katika harambee iliyofanyika jijini Arusha.

Mwenyekiti  wa Chama cha Wanaume Wazee Tanzania Joseph Laizer akieleza lengo la harambee ya kukiimarisha Chama hicho iliyofanyika jijini Arusha.

 Baadhi ya wanachama wa Chama cha Wazee Tanzania wakishiriki katika harambee ya kukiimarisha chama hicho, jijini Arusha.

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akivalishwa vazi la asili ya Kimasai na wana Kampeni ya SMAUJATA mkoa wa Arusha alipowasili mkoani hapo kwa lengo la kuongoza harambee ya kukiimarisha Chama cha Wanaume Wazee Tanzania iliyofanyika jijini Arusha.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM

About the author

mzalendoeditor