Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA AKERWA KUSUASUA UJENZI VETA MKOANI SIMIYU

Written by mzalendoeditor

Na Mathias Canal, WEST-Simiyu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) amekerwa na kusuasua kwa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi-VETA mkoani Simiyu.

Ameagiza wataalamu wote wa usimamizi wa chuo hicho ambao ni kutoka chuo cha ufundi Arusha waweke kambi mkoani Simiyu ili kukagua na kukamilisha haraka ujenzi huo.

Waziri Mkenda ameametoa maagizo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu leo tarehe 8 Octoba 2022.

“Tungependa kuona chuo cha ufundi Arusha kikisimamia kazi hadi watu binafsi wawatafute kwa ajili ya kwenda kusimamia ujenzi, lakini hapa sidhani kama wamefikia kiwango kizuri, wamejitahidi lakini hawajafikia kwahiyo siridhiki” Amekaririwa Waziri Mkenda

Chuo cha Ufundi stadi VETA-Simiyu ni miongoni wa vyuo vinne ambavyo vimesalia kukamilika ujenzi wake ili mikoa yote iwe na vyuo vya Ufundi VETA, Waziri Mkenda ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Simiyu, Rukwa, Njombe, na mkoa wa Songwe ambao fedha tayari zimepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Prof Mkenda amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora katika ujenzi wa Vyuo hivyo na kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa na serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.

Pia, Waziri Mkenda amesema kuwa changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafiri, serikali itaendelea kuzitatua.

Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa kwa sasa Wizara imejipanga kuanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika wilaya zote nchini hivyo kama ujenzi wa usimamizi wa vyuo vya mikoa unasuasua ni wazi kuwa kusimamia Wilaya zote nchini haitakuwa kazi rahisi.

About the author

mzalendoeditor