Featured Kitaifa

SH.BILIONI 23 KUJENGA WODI ZA WATOTO NJITI NCHINI.

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Bungeni Dodoma

Serikali imetenga kiasi cha Bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto njiti ili kupunguza vifo kwa watoto hao.

Hayo ameyasema Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel leo Bungeni kwenye mkutano wa Nane Kikao cha Sita Jijini Dodoma akiwa anajibu maswali ya nyongeza.

Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Cecilia Paraso Mbunge wa viti maalumu ameuliza nini mpango wa Serikali kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini.

“Nikuhakikishie kwamba Vifo vitokanavyo na uzazi vimekuwa vikipungua kutokana na juhudi za Serikali kujenga vituo vya Afya vya dharula kila mahali nchini ili wakina mama waweze kujifungua salama.” Amesema Dkt. Mollel

Akijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Suma Fyandomu Mbunge wa viti maalumu kuhusu ni lini hospital ya Rufaa Mbeya Meta itaanza kutumika kwa wakinamama wajawazito baada ya kufunguliwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akijibu swali hilo Dkt. Mollel amesema kuwa vifaa vitakavyotumika katika hospitali ya Rufaa Mbeya Meta vimeshanunuliwa vyenye thamani ya Bil. 2.1 na ndani ya miezi miwili vitafikishwa katika hospitali hiyo na kuanza kutumika.

Aidha Dkt. Mollel amesema juhudi kubwa zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha huduma bora za Afya zinatolewa nchini kwa kujenga vituo vya Afya na hospital za Rufaa nchini.

Pia, amesisitiza kwa kila mama mjamzito ajifungulie katika vituo vya Afya au Zahanati ili utambuzi uweze kufanyika na kumpa mtoto tiba stahiki pindi anapogundulika na tatizo.

Akijibu swali la pili la nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mariam Kisangi Mbunge wa viti maalumu juu ya watoto wanaozaliwa na Sikoseli.

Dkt. Mollel amesema hatua zimeshachukuliwa ili kupunguza tatizo hilo na Dawa za kuwasaidia watoto hao bajeti yake imeshatengwa MSD kununua na kuanza hatua za kusambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya kwa lengo la kuanza kugawa Dawa hizo kwa utaratibu maalumu.

Ameongezea pia, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Marekani tayari imetengenezwa programu maalumu inayoshughulikia matatizo ya watoto wenye Serimundu (Sikoseli) kuweza kuwasaidia.

About the author

mzalendoeditor