Rais wa mahakama ya Afrika mashariki Jaji Nestor Kayobera mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari unaoendelea mkoani Arusha.
……………………………………….
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Rais wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu Jaji Imani Aboud amesema kuwa uhuru na usalama wa wanahabari ni jambo muhimu kwani ni watu muhimu katika jamii yoyote inayoheshimu misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na haki za binadamu.
Ameyasema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari yaliyoandaliwa na UNESCO ambapo alisema kuwa jamii inawategemea wanahabari kuwa miongoni mwa watu wanaoleta amani kwa kutoa habari zinazohamasisha amani kuliko kutoa habari ambazo zinavunja amani.
“Usalama wao ni muhimu kwasababu tunawategemea wakati wowote iwe ni wakati wa uchaguzi, miradi ya maendeleo na nyinginezo kutoa habari zinazoleta amani kwasababu habari wanazozitoa katika vyombo vyao, wananchi wanazichukua kama walivyozitoa kwahiyo kama wakitoa habari ambazo hazielezi uhalisia na ukweli wa yale yanayoendelea wajue wanawapa habari ambazo sio sawa wananchi ambapo wanawaza kutoa maoni yanaweza kuvunja amani,” Alisema Jaji Imani.
Alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana na watafundishwa jinsi sauti mbalimbali za Afrika na nchi moja moja zinaweza kutumika kwa njia bora ya kuhakikisha kwamba waandishi wa habari wanakuwa na uhuru wa kutoa habari, kupewa habari, kusikilizwa na usalama wao.
“Majaji watafundishwa hapa wanapopata mashauri yanayohusu wanahabari wanawezaje kuzishughulikia kwa kuzingatia mambo gani , misingi gani na sana sana kwa kuangalia sheria zao za nchi pamoja na sheria zingine za kimataifa na mikataba ya kimataifa,” Alieleza.
Kwa upande wake Rais wa mahakama ya Afrika mashariki Jaji Nestor Kayobera alisema kuwa kuna kesi zinazohusu wanahabari ambazo zimeshasikilizwa na kutolewa maamuzi katika mahakama hiyo na wanaamini serikali zinafanya vizuri na wananchi kutoka katika nchi zote saba za jumuiya hiyo wanahaki ya kwenda katika mahakama ya Afrika mashariki na sio lazima wapite katika mahakama ya ndani ya nchi zao.
“Sheria ya mahakama hiyo kifungu cha 38(3) inasema nchi yoyote lazima iheshimu uamuzi wa mahakama hivyo mahakama hiyo ikishatoa maamuzi ni lazima iende kuangalia kama uamuzi huo kama umetekeleza ambapo kama haujatekelezwa mshitaki anarudi mahakamani na kwakuwa maamuzi yote waliyotoa kutokana na kesi zinazohusu wanahabari yametekelezwa kwasababu walikuwa wameshitaki hawajarudi mahakamani,” Alisema Jaji Kayobera.
Naye Jaji David Ngunyale mwakilishi wa mkuu wa chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto alisema kuwa mafunzo hayo ni kwaajili ya wadau wa utoaji haki kuweza kuelewa juu ya uhuru wa habari au uhuru wa kujieleza, kuwa ni jinsi gani unahusiana na masuala ya utoaji haki ili wananchi waweze kupata taarifa zinazostahili kwani wanahaki ya kupata habari ambapo katika suala Hilo mahakama ni lazima iwe na mazingira rafiki yanayowezesha watu kupata habari.
“Mahakama sasa hivi Ina mifumo ambayo inawawezesha wananchi kufika mahakama lakini pia kupata taarifa sahihi kwa wakati sahihi ndio maana tunajitahidi kuhakikisha majaji na mahakimu wanajengewa uwezo juu ya umuhimu wa suala hili, lakini pia tukielewa vizuri kuhusu usalama wa wanahabari kwa kuzingatia utawala wa sheria tutajua kwanini wapo kwasababu wanahaki ya kuripoti yanayoendea,” Alisema.
Mkuu wa mradi wa uwajibikaji wa wanahabari kutoka UNESCO Mehdi Benchelah alisema kuwa uhuru wa kujieleza imekuwa ni changamoto kubwa Duniani ambapo kumekuwa na kesi nyingi za wanahabari wakati mwingine wanauwa jambo linaloathiri tasnia nzima ya habari na wananchi kwa ujumla kwa kukosa uhuru wa kupata habari na UNESCO tumeona ni vyema kuwapa mafunzo haya watendaji wa mahakama ili kuwapa uelewa juu ya utawala wa kisheria na uhuru wa kujieleza ambapo wanapadishana mawazo ni vipi nchi za ulaya na za Afrika zinafanya ili kuweza kusimamia suala hili.
Mkuu wa mradi wa uwajibikaji wa wanahabari kutoka UNESCO Mehdi Benchelah akiongea na waandishi wa habari katika mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari unaoendelea mkoani Arusha.
Rais wa mahakama ya Afrika mashariki Jaji Nestor Kayobera mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari unaoendelea mkoani Arusha.
Jaji David Ngunyale mwakilishi wa mkuu wa chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto akiongea na wanahabari katika mafunzo hayo.
Rais wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu Jaji Imani Aboud akiongea na waandishi wa habari mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari unaoendelea mkoani Arusha.
baadhi watendaji wa mahakama mbalimbali za Afrika na nchi za Afrika wakifuatilia jambo katika mafunzo ya watendaji wa mahakama kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari unaoendelea mkoani Arusha.