Featured Makala

TANZANIA MSHIRIKI MADHUBUTI WA TAMASHA LA JAMAFEST 

Written by mzalendoeditor

Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko akiongea na Wanafunzi wa shule ya msingi Mwanyahina kutoka wilaya ya Meatu mkoani Simiyu ambao ni washindi wa kwanza wa mashindano ya UMITASHUMTA katika fani ya ngoma 2022 mara baada ya kutumbuiza kwenye Tamasha la JAMAFEST hivi karibuni nchini Burundi.

………………………………………

Na Eleuteri Mangi, WUSM

Tanzania mara zote imekuwa ikishiriki madhubuti wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) kwa kishindo na bashasha ambalo ni nyenzo adhimu ya kukuza ushirikiano wa kijamii na kitamaduni miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Tamasha hilo hufanyika kwa mzunguko kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limekuwa fursa na jukwaa maridhawa kwa wasanii na wajasiriamali kuonesha na kuuza kazi zao na hivyo kujipatia kipato na kukuza uchumi wa nchi linapofanyika tamasha hilo pamoja na wageni wanaoleta bishara zao. 

Mratibu wa JAMAFEST Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Leah Kihimbi anasema mara zote Tanzania inatia fora kwa kuwa na wasanii wengi wanaotumbuiza kwenye tamasha hilo.

“Nchi yetu mara zote imekuwa ikifanya vizuri sana kwenye Tamasha hili, mwaka huu kuna washiriki wengi zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki, matahalani mwaka huu tumepeleka vikundi 10 ikiwemo ngoma za asili, muziki wa taarabu, singeli, kughani mashairi, watumishi wa umma. wajasiriamali pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi ambao walileta burudani ya ngoma” amesema Bi. Leah.

Ni dhahiri ushiriki wa Tanzania kwenye Tamasha la JAMAFEST 2022 Bujumbura nchini Burundi umekuwa wa kishindo kwa kuwa na washiriki wengi ambao idadi yao ni takriban 200 wakiwemo watumishi wa umma, wajasiriamali, wasanii katika fani mbalimbali za Sanaa na Utamaduni pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Mwanyahina kutoka wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wajasiriamali katika Tamasha la JAMAFEST 2022 kutoka Tanzania Maimuna Chiputa ambaye pia mfanyabishara kutoka wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara anasema tamasha limewasaidia kufungua milango ya bishara nchini Burundi na limekuwa kichocheo kikuu cha ushirikiano wa kikanda kwa kuwasaidia wafanyabiashara kuongeza wigo kwa kupata masoko ya kupeleka bidhaa zao kwenye nchi linapofanyika tamasha na baadhi ya wafanyabishara wamepata soko la bidha zao nchini Burundi na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumepata fursa nyingi, biashara zetu zimeuzika hapa Burundi na nje ya Burundi, wamenunua watu kutoka Kongo, Rwanda na nchi nyingine wamechukua. Biashara ni nzuri watu wameuza, kubwa zaidi watu wamepata oda ya kuleta bidhaa hapa Burundi, tumefurahia sana hili tamasha” amesema Maimuna. 

Tanzania ilipongezwa kwa kuleta wajasiliamali wengi zaidi na bidhaa zenye ubora ambazo zilivutia mamia wa watu waliojitokeza kutembelea mabanda ya wajasiliamali wa Watanzania. 

Baadhi ya bidhaa zilizoletwa na wajasiliamali kutoka Tanzania ni  pamoja na korosho, mchele, pilipili, viungo vya chakula kama vile tea masala, pilau masala, mchuzi mix, chicken masala, dagaa wa Zanzibar, unga wa mihogo, unga lishe, unga wa sembe na dona, asali, Dodoma wine, mabibo wine, nguo za batiki za kike na kiume, madawa ya asili, vikapu, mwani na bidhaa zinazotokana na mwani kama sabuni ya kuogea, kufulia na mafuta ya kupaka ngozi na  nywele, mama lishe, urembo wa shanga, picha za vivutio vya wanyama waliopo Tanzania na viatu vya wazi vya ngozi.

Maonesho ya bidhaa hizo yaliongeza na kupanua wigo wa fursa za masoko ya kazi na utamaduni, Sanaa na ubunifu kwa Watanzania na kujenga mtandao mpya wa uhusiano wa kibiashara baina ya Watanzania na Wanajumuiya  wa Afrika Mashariki wa ndani na nje ya Jumuiya. 

Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC kukaa Septemba 2011 na kuiagiza Sekretarieti ya jumuiya hiyo kuandaa matamasha ya mara kwa mara ya aina hiyo ambapo kwa mara ya kwanza pazia lilifungua Februari 11 hadi 17, 2013 katika jiji la Kigali nchini Rwanda kuwa mwenyeji wa tamasha hilo, huku Kenya ikipokea kijiti 2015, Uganda 2017, Tanzania 2019 na Burundi 2022. 

Chimbuko la Tamasha la JAMAFEST ni Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Machi 19 hadi 26, 2010 (EAC/CM/20/Maelekezo 71) ambao umekuwa chachu ya kufanyika kwa matamasha ya Sanaa na Utamaduni, mashindano ya michezo na Kongamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yakishirikisha pia sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na washirika wa Maendeleo miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo. 

Aidha, uamuzi wa Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika Septemba 5 hadi 9, 2011 kwa Baraza la 9 la Kisekta la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo wa kufanya Tamasha la Sanaa na Utamaduni na Michezo la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nchi Wanachama kwa zamu unaendelea kuwa msingi thabiti wa kufanyika Tamasha la JAMAFEST.

Uamuzi huo unapata mamlaka kupitia Ibara ya 119 ya Mkataba wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo kwa pamoja ziliazimia kukuza ushirikiano wa karibu baina yao katika sekta ya Utamaduni na Michezo.

Tamasha la JAMAFEST ni fursa kwa watanzania na wananchi wa jumuiya hiyo kwa ujumla ambapo sasa wananufaika na kazi za Sanaa za muziki, ufundi wa uchoraji, uchongaji, fasihi, sanaa ya maigizo, ubunifu na kazi nyingine za Sanaa ili kuhifadhi, kulinda na kuendeleza urithi wa kitamaduni, kukuza utambulisho na kuimarisha utangamano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Elibariki Maleko akiongea na Wanafunzi wa shule ya msingi Mwanyahina kutoka wilaya ya Meatu mkoani Simiyu ambao ni washindi wa kwanza wa mashindano ya UMITASHUMTA katika fani ya ngoma 2022 mara baada ya kutumbuiza kwenye Tamasha la JAMAFEST hivi karibuni nchini Burundi.

Wageni mbalimbali wakitembelea mabanda ya wajasiriamali wa Tanzania wakati wa Tamasha la JAMAFEST hivi karibuni nchini Burundi.

About the author

mzalendoeditor