Featured

MAKAMU WA RAIS ATETA NA WATANZANIA WAISHIO NEW YORK MAREKANI

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiaganana viongozi wa Jumuiya ya  watanzania waishio Jijini New York nchini Marekani, mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania Jijini New York.

………………………………………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya  watanzania waishio Jijini New York nchini Marekani, Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania Jijini New York.

Akizungumza na Watanzania hao, Makamu wa Rais amewapongeza kwa jitihada wanazofanya za kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali. 

Amesema serikali ya awamu ya sita inatambua mchango wa wana diaspora hao na itaendelea kuunga mkono jitihada wanazofanya.

Makamu wa Rais amewasihi watanzania waishio Marekani na duniani kote kwa ujumla kuhakikisha wanaishi kwa kufuata sheria katika nchi hizo na kujiepusha na vitendo vya kihalifu vitakavyoharibu taswira ya Tanzania. 

Aidha amewaasa kuendelea kuitangaza vema Tanzania, kuvutia wawekezaji pamoja na wao kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini. 

Pia amewataka kufanya juhudi za kutafuta masoko ya bidhaa na malighafi za Tanzania katika nchi wanazoishi kwa manufaa ya watanzania waliowengi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kutokana na lugha ya Kiswahili kuanza kutumika katika Jumuiya mbalimbali kama lugha rasmi, Diaspora wanapaswa kuendeleza lugha hiyo kwa kuitangaza na kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili katika maeneo waliopo. 

Makamu wa Rais amesema suala la utangazaji wa lugha ya Kiswahili linapaswa kwenda sambamba na kutangaza utamaduni wa taifa la Tanzania pamoja na vivutio vizuri vilivyopo.

Amesema serikali itaendelea kuleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania wote na kueleza kwamba serikali imefanya jitihada katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya kwa ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba, sekta ya elimu pamoja na ujenzi wa mindombinu ikiwemo ya barabara.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema Wizara ya Mambo ya Nje ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sera ya mambo ya nje ambayo inatambua mchango wa diaspora.

 Aidha amesema Wizara itazindua kanzu data, ambayo itawezesha wanadiaspora kutambulika popote walipo duniani.

Awali Mwanzilishi wa Jumuiya ya Watanzania Jijini New York Profesa Estomiah Mtui ameishukuru serikali kwa utaratibu maalum uliowawezesha kupata vitambulisho vya taifa pamoja na kuendelea kushughulikia suala la hadhi maalumu kwa diaspora. 

Prof Mtui amesema Jumuiya itaendeleza ushirikiano na kuchangia maendeleo nchini Tanzania kwa kutambua kwamba ni wajibu wa kila mtanzania kuchangia maendeleo kwa taifa lake.

Makamu wa Rais yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Jumuiya ya  watanzania waishio Jijini New York nchini Marekani, Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania Jijini New York.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiaganana viongozi wa Jumuiya ya  watanzania waishio Jijini New York nchini Marekani, mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika katika Ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania Jijini New York.

About the author

mzalendoeditor