Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizinduzi mradi wa Maji Makongolosi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
…………………………………………..
Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Chunya- Mbeya
Mradi wa maji uliopo Makongolosi wilayani Chunya mkoani Mbeya unaohudumia wakazi 25000 ambapo ni sawa na asilimia 70 unatajwa kutatua changamoto ya maji ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza leo, wilayani hapo mara baada ya kuzindua mradi huo uligharimu shilingi bilioni 2.89, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa alifanya ziara wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na kuwaahidi wananchi wa eneo hilo kuwa angetatua changamoto hiyo ya maji.
“Tulikuja na Ilani tukasema ahadi zetu tukiahidi ndani ya Serikali kuwa tutazitekeleza. Mimi kama mama natambua changamoto hiyo na nimesema nitahakikisha natatua changamoto hiyo ya maji, ahadi yangu kwenu ni kuwa mwaka 2025 upatikanaji wa maji vijijini utafikia asilimia 85 na mijini asilimia 95 sina shaka tutafika kwa kuwa fedha zipo, watendakazi wapo na wameimarika hivyo kazi itaenda vyema” . Amesema Rais Samia
Aidha, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) katika Wlaya ya Chunya, Mhandisi Ismail Ismail amesema kuwa kabla ya mradi huo upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 37 na baada ya mradi umefikia asilimia 43.
“Mkakati wetu ni kuwa katika bajeti ya mwaka 2022 hadi 2023 tumejipanga kupeleka maji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na mradi huu na tutaanza na uandaaji wa miundombinu, lakini pia kabla ya mradi huu upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 10 na hivi sasa ni asilimia 70.
Naye mkazi wa Makongolosi, Bw. Juma Bakari amesema kuwa kabla ya mradi huu wanawake walipata shida zaidi kwa kwenda kutafuta maji usiku na kwa kutumia muda mrefu.
“ Wakina mama walikuwa wakiamka saa kumi alfajiri kutafuta maji visimani na kwa masaa mengi na hivyo ilitupa usumbufu mkubwa kwenye familia zetu lakini sasa hivi maji yameanza kutoka mfululizo tunaishukuru sana Serikali” Amesisitiza Bw. Bakari
Vilevile, Beatrice Bilali mkazi wa eneo hilo nae ameongeza “Binafsi kwenye maji tunamshukuru Mungu, tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa vile amejua umuhimu wa maji, tuliteseka sana ametutua ndoo kichwani kilio chetu amesikia”