Featured Kitaifa

UGANDA WATEMBELEA MRADI WA GESI ASILIA KINYEREZI,WAIPONGEZA SERIKALI KWA KAZI ILIYOFANYIKA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (kulia), Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda, Mhandisi Peter Lokeris (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maliasili wa Uganda, Emmanuel Otara (wa pili kushoto) na Balozi wa Ubalozi wa Uganda, Fred Mwesigye (kushoto) wakifatilia mada wakati wa kikao cha ujumbe wa Uganda nchini Tanzania kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati

Meneja wa Kampuni inayohusika na Gesi ( GASCO) ambayo ni Kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Mhandisi Baltazar Mroso( kulia) akitoa maelezo kwa ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha Kupokea Gesi Asilia cha Kinyerezi Julai 21,2022, Dar es Salaam.

Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, cha Kinyerezi II, Mhandisi John Mageni (katikati) pamoja na ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo hicho Julai 21, 2022, Mkoani Dar es Salaam.

Mmoja wa wasimamizi wa Kituo cha Kupokea Gesi Asilia cha Kinyerezi(kushoto), akitoa maelezo kwa ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo hicho Julai 21,2022, Mkoani Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (katikati),akieleza jambo kwa ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo kuzalisha umeme cha Kinyerezi II Julai 21,2022, Mkoani Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo kuzalisha umeme cha Kinyerezi Julai 21, 2022, Mkoani Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, (kulia), akijadili jambo na Balozi wa Ubalozi wa Uganda Fred Mwesigye (kushoto), wakati wa ziara ya Ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, walipotembelea Kituo kupokea Gesi cha Kinyerezi  Julai 21,2022, Mkoani Dar es Salaam.

Meneja wa Kampuni inayohusika na Gesi ( GASCO) ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Mhandisi Baltazar Mroso( kulia) akiwaonesha mfumo wa gari inayotumia Gesi Asilia kwa ujumbe wa Uganda waliofika nchini kujifunza masuala mbalimbali katika sekta ya Nishati, wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi Julai 21,2022, Dar es Salaam.

…………………………..

Na Zuena Msuya DSM

Ujumbe kutoka nchini Uganda umeipondeza Serikali ya Tanzania na kufurahishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi Mkoani Dar es salaam, baada ya kutembelea mradi huo.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka nchini Uganda uliohusisha Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda, Mhandisi Peter Lokeris na Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maliasili nchini humo walipotembelea Mradi wa Kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezij Julai 21,2022.

Ujumbe wa Uganda uko nchini kwa ziara ya siku sita kwa lengo la kujifunza na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya Nishati,kuanzia  Julai 19 hadi 24, 2022 katika Mkoa wa Dar es salaam na Tanga.

Mhandisi Mramba amesema kuwa wageni hao wameona na kufurahishwa na kazi kubwa ya uwekezaji iliyofanyika katika kutekeleza Mradi wa Kinyerezi, na kwamba wameipongeza serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi huo adhimu kwa nchi za Afrika Mashariki.

Amesema ujio wao ni uthibitisho tosha kuwa nchi hizo mbili sasa ziko tayari kushirikiana katika rasilimali ya gesi asilia inayochimbwa hapa nchini.

Aliweka wazi kuwa, ikumbukwe kuwa mwezi Mei mwaka huu, Viongozi Wakuu wa nchi hizo mbili, Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Kabuta Museveni walifanya mazungumzo juu ya ujenzi wa bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Tanzania hadi Uganda ili kuiwezesha nchi hiyo kuzalisha umeme unaotakana na gesi pamoja na matumizi mengine.

Na walikubalina kuwa bomba hilo likijengwa lipite katika maeneo yenye watu ili gesi hiyo iendelee kutumika na baadaye lifike Uganda.

Alisema mazungumzo hayo yalikwenda vizuri, ambapo sasa Tanzania imeanza kufanya upembuzi yakinifu ili kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda Mhandisi Peter Lokeris na ujumbe alioambata nao wamepongea serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa Kinyerezi ambao umesababisha nchi ya Tanzania kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.

Alisema mradi huo pia umesababisha viwanda kuongezeka kwa wingi nchini humo kwa kuwa wawekezaji wanauhakika wa kufanya uzalishaji katika viwanda vyao muda wowote kutokana na kuwa na umeme na hiyo umechangia kasi kubwa ya ukuaji wa viwanda nchini humo.

Alifafanua kuwa Uganda inatamani kuwa na mradi kama huo nchini humo, na kwamba baada ya kuona kilichofanyika wataisisitiza serikali yao kuharakisha mchakato wa utekelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Tanzania hadi nchini mwao kwa kuwa wameshuhudia manufaa makubwa ya uwepo wa mradi huo Tanzania.

Mhandisi Lokeris alijinasibu kwa kusema kuwa endapo mradi huo utatekelezeka Uganda nchi hiyo itakuwa kiuchumi kwakuwa watakuwa na uhakika wa kuwa na umeme mwingi na wa kutosha kuwezesha wawekezaji wengi kuwekeza nchini humo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maliasili wa Uganda, Emanuel Otara alisema kuwa kamati hiyo imekuja kuangalia miundombinu ya gesi ambayo tayari viongozi wakubwa wa nchi hiyo wamezungumza na kuona namna ambavyo Tanzania imefanikiwa.

Hakika tumefurahi sana kuona kuwa inawezakana mradi kama huo kufanyika Uganda na kuleta manufaa zaidi kwa taifa hilo kiuchumi.

Baada ya kuona uwekezaji huo, wabunge tumeridhia mradi huo ufike Uganda na tumeelezwa kuwa mazugumzo yanaendelea vizuri  juu ya tekelezaji wake, tuko tayari kuupokea.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula ameishauri serikali kuwa kwa sasa kama taifa kuwawezesha wataalam wa ndani waliotekeleza mradi wa Kinyerezi watumike kujenga miradi ya namna hiyo katika ukanda wote wa Afrika kutokana na uzoezi walionao.

Alisema Kampuni ya GASCO ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya petroli nchini (TPDC), itumike zaidi katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Tanzania hadi Uganda kwa kuwa wataalam hao wameonyesha umahiri mkubwa katika kutekeleza mradi wa Kinyerezi.

Ujumbe huo umezishauri nchi zingine za Afrika Mashariki, kuja Tanzania kujifunza ili kuona hatua ya maendeleo yaliopigwa na nchi hiyo katika miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo umeme, mafuta na Gesi.

About the author

mzalendoeditor