Featured Kitaifa

SERIKALI KUJENGA VITUO 19 VYA ASKARI WA WANYAMAPORI

Written by mzalendoeditor

  

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana,akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya mpango na bajeti ya Wizara yake ya mwaka 2022- 2023 na Jinsi Vitakavyowanufaisha Wananchi leo Julai 19,2022 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana,akijibu Maswali mbalimbali yaliyoulizwa na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)  wakati akielezea utekelezaji wa vipaumbele vya mpango na bajeti ya Wizara yake ya mwaka 2022- 2023 na Jinsi Vitakavyowanufaisha Wananchi leo Julai 19,2022 jijini Dodoma.

……………………………..

Na Odilo Bolgas-DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022 2023 imepanga  kujenga vituo 19 vya kambi za askari wa wanyamapori ili kukabiliana na uharibifu mazao ya wananchi unaofanywa na wanyamapori wakali ambao wamekuwa na tabia ya kuingia kwenye makazi ya watu.

Akizungumza lna Waandishi wa habari leo Julai 19,2022 Jijini Dodoma Waziri wa Maliasili na Utalii  Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana  wakati akitoa taarifa  kuhusu vipaumbele vya mpango na  bajeti kuu ya mwaka 2022/2023 ya wizara hiyo na jinsi vitakavyowanufaisha wananchi.

Amesema kutokana na uharibifu huo unaofanywa  na Wanyamapori hao pia watatoa elimu kwa wananchi  juu ya mbinu bora za kukabiliana na wanyamapori waharibifu pamoja na kujenga kambi hizo za askari wa wanyamapori.

Amebanisha kuwa wizara itatoa elimu juu ya mbinu rafiki za kukabiliana na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na kuwawezesha vitendea kazi vya kukabiliana nao.

“Wizara itatoa elimu juu ya mbinu rafiki za kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu tutawezesha utoaji elimu na vitendea kazi na tutaanza na maeneo ambayo vitendo hivyo vimekithiri” amesema Balozi Pindi.

Amebainisha  Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na wananchi hao wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi pamoja na wizara zingine za kisekta ili kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi ya vijiji kwa lengo la kuepusha migongano.

Amesema wizara itaanza matumizi ya mfumo wa kieletroniki kwa ajili ya kupokea taarifa za kifuta jasho ambacho ni pole ambayo inatolewa kwa wananchi kutokana na madhara yaliyosababishwa na wanyamapori hao .

Aidha kuhusu kuendeleza program ya the royal tour wanaendelea na kasi ya kutangaza utalii kitaifa na kimataifa kwa kuibua masoko mapya ya utalii kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii

Katika hatua nyingine  amesema katika kuboresha huduma za malazi  na chakula nchini kwa mwaka 2022/23 wizara  itaanza kutumia mfumo wa kieletroniki wa kupanga huduma hizo katika madaraja ya ubora wa nyota .

Amesema  kuwa katika kuendeleza kampeni za kutunza mazingira wizara itaandaa mipango ya usimamizi wa misiti 57 yenye ukubwa wa hekta 1,703,202  na kufanya mapitio ya usimamizi wa misitu ya hifadhi 111 pamoja na kuhakiki kupima mipaka ya misitu 133 na kuhakiki mipaka yenye urefu wa kilomita 33,107.

Amesema Serikali inakusudia kuanza ujenzi wa makumbusho ya Marais waliopita makumbusho yatakayojengwa jijini Dodoma lengo likiwa ni kusaidia kuonyesha kwa jamii mchango wa Marais katika Nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kipindi wakiwa madarakani.

Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wizara hiyo imeidhinishiwa na bunge jumla ya shilingi bilioni 670.85 katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi mengine.

Pia katika bajeti hiyo Wizara imepanga kuboresha miondombinu katika maeneo ya hifadhi kwa kujenga na kukarabati bara bara na madaraja katika maeneo ya hifadhi mbalimbali hapa nchini.

About the author

mzalendoeditor