Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa harambee ya kampeni ya GGM Kili Challenge inayotarajiwa kufanyika tarehe 14 Julai, 2022 mkoani Kilimanjaro. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Steven Kagaigai.
…………………………………
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene anatarajiwa kuzindua harambee ya Kampeni ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2022 inayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini na kushirikisha wadau kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI.
GGM Kili challenge ni mfuko ulioanzishwa mwaka 2002 na kampuni ya GGM. Kampeni hii inasimamiwa na GGM kwa kushirikiana na TACAIDS ikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.
Malengo ya sifuri tatu yanamaanisha kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro jana, Mkuu wa mkoa huo, Steven Kagaigai alisema harambee inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 14 Julai, 2022 katika hotel ya Weruweru River Lodge iliyopo wilayani Hai mkoani humo.
Alisema uchangiaji wa fedha hizo unalenga zaidi jamii zilizoko kwenye mazingira hatarishi ya maambukizi ya VVU na kupunguza athari za UKIMWI.
Alisema kampeni hiyo hufanyika kila mwaka na ilianza rasmi tangu mwaka 2002 na huu ni katika mwendelezo wa ukusanyaji fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini sambamba na kutoa fursa ya utalii katika mlima Kilimanjaro.
“Shughuli kubwa katika siku hii ni kufanya harambee “Fund raising” ya uchangishaji fedha kutoka kwa wadau ambao watahudhuria tukio hilo. Tukio hilo litafuatiwa na tukio la kuwasindikiza wapanda mlima na waendesha baiskeli (Flag Off) siku ya pili yake tarehe 15 Julai 2022, katika Lango la Machame Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
“Tarehe 21 Julai 2022 litafanyika tukio la kuwapokea wapanda mlima na waendesha baiskeli kuzunguka Mlima Kilimanjaro katika Lango la Mweka, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa George Simbachawene Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),” alisema.
Alisema katika zoezi hilo la kupanda mlima, huduma mbalimbali zitatolewa zikiwamo elimu na upimaji wa VVU, chanjo ya UVIKO – 19 pamoja na uchangiaji wa damu.
“Hivyo natoa hamasa kwa wananchi wote kujitokeza kupata huduma hizi zitakazotolewa bila malipo. Pia wadau mbalimbali waliopo mkoani kwetu hata nje ya mkoa, makampuni, wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla ndani na nje ya Mkoa wetu wanakaribishwa kujitokeza kwa wingi katika matukio haya muhimu. Mjitokeze kwa wingi kupima na kujua afya zenu sambamba na kuchanja chanjo ya UVIKO 19 katika lango la Machame na Mweka kuanzia tarehe 15Julai 2022,” alisema.
Aidha, Meneja Mwandamizi anayehusika na ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma alisema katika tukio hili la upandaji wa Mlima Kilimanjaro, njia itakayotumika ni ile yenye changamoto nyingi “Njia ya Machame” ambayo imependekezwa mahsusi kuonesha jinsi mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI yalivyo na changamoto.
“Lakini pia, kupitia tukio hili tutaongeza hamasa ya utalii ya upandaji Mlima Kilimanjaro kwa watalii wa ndani, Afrika na ulimwenguni kote,” alisema.
Alisema mwaka huu wameendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, hivyo GGM kwa kushirikiana na TACAIDS wanatarajia kuanza kampeni ya kupanda mlima ifikapo Julai 15 hadi Julai 21 mwaka huu.
“Tunawakaribisha sana wadau wetu na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki kampeni hii,” alisema Bw Ndoroma.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.
GGM Kili Challenge imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli zaidi ya 700 kutoka mabara 6 na zaidi ya nchi 20.
Wakati Mkurugenzi Mkuu TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, UKIMWI bado ni tatizo nchini.
Alisema takwimu zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya VVU hususan kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi. Hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya Watanzania wanaoshi na virusi vya UKIMWI nchini imefikia watu 1,700,000 na maambukizo mapya kwa mwaka ni watu 68,000.
Kupitia kampeni ya GGM Kilimanjaro challenge, taasisi mbalimbali zimenufaika kwa kupata fedha za kutekeleza shughuli za mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini. Kwa mfano, mwaka 2020 Mfuko wa Kilimanjaro Challenge ulitoa fedha taslim Sh milioni 800 kwa taasisi 20 zisizo za kiserikali.
Asasi hizo zimetekeleza miradi mbalimbali iliyowalenga vijana, watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, watoto yatima na waliopo kwenye mazingira magumu. Zaidi ya watu 1,000 wamenufaika kutokana na fedha hizo.