Featured Kitaifa

WANANCHI DODOMA WAVUTIWA NA TUNDA LA KWEME BANDA LA NELSON MANDELA

Written by mzalendoeditor

Mbunge wa Moshi Vijijini Profesa  Patrick Ndakidemi (Kushoto) akipata maelezo kuhusu tunda la Kweme kutoka kwa Mtafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wa Chuo Kikuu  cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia Cha Nelson Mandela (NM-AIST) Bi . Philipina Shayo  (kulia) alipotembelea Banda la Chuo hicho katika  Maonyesho ya  Wiki ya Ubunifu Tanzania  leo Mei 18 ,2022 uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Wanafunzi wa Dodoma Sekondari (Kushoto) wakimsikiliza Mtafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wa Chuo Kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia Cha Nelson Mandela (NM-AIST) Bi . Philipina Shayo  (kulia)  aliyekuwa akiwaelezea faida zitokenazo na mbegu za tunda la kweme  wakati wa  Maonyesho ya  Wiki ya Ubunifu Tanzania  leo Mei 18 ,2022 uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Wanafunzi wa  Shule ya Kimataifa ya Msingi Feza ya Jijini Dodoma (Kushoto) wakipata maelezo kuhusu mbegu za tunda la Kweme kutoka kwa Mtafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wa Chuo Kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) Bi . Philipina Shayo  (kulia) alipotembelea Banda la Chuo hicho katika  Maonyesho ya  Wiki ya Ubunifu Tanzania  leo Mei 18 ,2022 uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Wakazi wa Dodoma (Kushoto) wakipata maelezo ya kina  kuhusu tunda la Kweme kutoka kwa Mtafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wa Chuo Kikuu  cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia Cha Nelson Mandela (NM-AIST) Bi . Philipina Shayo  (kulia) walipotembelea Banda la Chuo hicho katika  Maonyesho ya  Wiki ya Ubunifu Tanzania  leo Mei 18 ,2022 uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Mwonekano wa Tunda la Kweme na mbegu zake  mmea uliofanyiwa utafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kutoka  Chuo  Kikuu Cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) Bi . Philipina Shayo   katika  Maonyesho ya  Wiki ya Ubunifu Tanzania  leo Mei 18 ,2022 uwanja wa Jamhuri Dodoma.

……………………………………………

Wananchi wa Jiji la Dodoma wavutiwa na tunda la kweme linalopatikana katika Banda la Chuo Kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) leo Mei 18, 2022 kwenye maonyesho ya Wiki ya Ubunifu wa Tanzania yanayofanyika katika uwanja wa Jamhuri.

Wananchi hao walifanikiwa kupata maelezo ya kina kuhusu tunda hilo,  kutoka kwa Mtafiti na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kutoka NM-AIST  Bi . Philipina Shayo  kuwa, mmea huo wa asili  utambaao  ni jamii ya matango  ambapo hulimwa nchini Tanzania katika  mkoa wa Tanga, Arusha, Mbeya, Ruvuma,Morogoro, Kilimanjaro na Zanzibar pamoja na  nchi  jirani za Msumbiji  na Uganda.

“tunda hili lina uzito kati ya  gramu 7 hadi 20 ,likiwa na mbegu au karanga zipatazo 80-200 nadani yake ambazo zikihifadhiwa kwenye mazingira makavu zinaweza kukaa hadi miaka nane bila kupoteza ubora wake” alisema Bi. Philipina

Alizidi kueleza kuwa,  mbegu za tunda la Kweme zina faida nyingi kwa jamii  ikiwemo kutumiwa na wakina mama wanaonyonyesha, hutengeneza sabuni, mishumaa na urembo  wa ngozi na nywele.

Amefafanua zaidi kuwa, tunda hilo hutibu ugonjwa wa Jongo (rheumatism) , hutibu matatizo ya tumbo, husaidia kupunguza hewa ya ukaa ambayo ina madhara kwa binadamu na mazingira .

Bi. Philipina ameongeza kuwa,  mashudu ya tunda hilo hutumika kutengenezea vyakula vya mifugo pamoja na kuboresha mazingira na udongo hususani kwenye kilimo mseto haswa maeneo ya milimani kama vile Kilimanjaro, Meru na Upare.

Aidha Bi. Philipina aliwafafanulia wananachi hao kuwa katika kila mbegu ya kweme yenye uzito wa kilogramu 100 husaidia  binadamu kupata mafuta 28%, Protini 25%, Wanga  5%, Asidi ya Mafuta (linoleic acid)  47% pamoja na madini ya Zinki, Selenium, Potasiamu,Fosforasi, Kalsium, Chuma, Sodiam na Magneziamu.

Bw.Yusuph Nandonde mwananchi aliyepata fursa ya kutembelea Banda la Nelson Mandela ameeleza kunufaika na elimu aliyoipata kutoka kwa Mtafiti huyo kwa kuwa hapo awali alizoea kuziona na kula mbegu zake bila kulifahamu tunda linalotoa mbegu hizo.

“Hakika mtembea bure, siyo sawa na mkaa bure nimekuja na nimeondoka na kitu cha thamani sana ,hongereni kwa kutoa elimu hii muhimu  kwa jamii yetu alisema” Bw. Yusuph

Chuo Kikuu cha Afrika  cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela ni moja ya  Taasisi za Vyuo Vikuu iliyoshiriki Maonyesho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania iliyoanza tarehe 16 Mei 2022 katika Uwanja wa Jamhuri  Dodoma.

About the author

mzalendoeditor