Featured Kitaifa

WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI SIMAMIENI UTAWALA BORA-MAJALIWA

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua mafunzo ya Utawala Bora kwa watendaji wa kata na vijiji, kwenye ukumbi wa Ghala la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Lindi 

Watendaji wa Kata na vijiji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipofungua mafunzo ya Utawala Bora kwa watendaji wa kata na vijiji, kwenye ukumbi wa Ghala la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Lindi Aprili 14, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa kata na vijiji nchini wasimamie vema utawala bora na utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro sambamba na ushirikishaji wananchi katika maamuzi na mipango ya maendeleo.

“Uwazi ni moja ya msingi wa utawala bora, viongozi hakikisheni wananchi wanapata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo. Toeni taarifa za mapato na matumizi. Hii itaondoa hisia za uwepo wa ubadhirifu na mtajenga imani kwa wananchi.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Aprili 14, 2022) wakati akifungua mafunzo ya utawala bora kwa Watendaji wa Kata na Vijiji wilayani Ruangwa. Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Hanns Seide yanafanyika katika ukumbi wa Ghala la Halmashauri.

“Nendeni mkatambue makundi yote katika jamii ili kila mwananchi atambue nafasi yake ya kuwa yeye ni sehemu ya jamii na pia ana mchango na haki ya kupata maslahi. Utatuzi wa migogoro katika maeneo yenu ya utendaji uwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji hao wahamasishe umuhimu wa mbio za mwenge kama moja ya alama za nchi yetu. “Wananchi wafahamishwe historia ya mwenge ili waweze kuuthamini kama njia moja ya kumuenzi Baba wa Taifa letu.”

“Sote tunafahamu mbio za mwenge pamoja na mambo mengine zimekuwa zikitumika kukagua miradi inayotekelezwa katika halmashauri na kuweka mawe ya msingi katika baadhi ya miradi. Tuwaelimishe wananchi wasikubali kushawishiwa kuipinga historia ya Taifa letu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza Watendaji wote wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa wasimamie matamko na maelekezo yote ya viongozi wajuu yakiwemo maandalizi ya zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema watendaji hao wana jukumu la kuhamasisha wananchi sambamba na kushiriki kikamilifu katika mchakato wote wa maandalizi. “Wananchi wako katika vijiji na vitongoji vyenu wapeni elimu sahihi wawe na utayari wakati wa kuhesabiwa.”

About the author

mzalendoeditor