Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI RIDHIWANI AWAONYA WENYEVITI MABARAZA YA ARDHI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza katika kikao kazi na mafunzo cha wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya pamoja na Wasajili Wasaidizi mkoani Tanga.

Sehemu ya washiriki wa kikao kazi na mafunzo cha Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pamoja na Wasajili wasaidizi wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Ridhiwani Kikwete wakati wa ufunguzi wa kikoa hicho 

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akizungumza kwenye kikao kazi na mafunzo cha wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya pamoja na Wasajili Wasaidizi mkoani Tanga

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stella Tullo akizungumza katika kikao kazi na mafunzo cha wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya pamoja na Wasajili Wasaidizi mkoani Tanga 

Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa akizungumza katika kikao kazi na mafunzo cha wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya pamoja na Wasajili Wasaidizi mkoani Tanga 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akisalimiana na mmoja wa wenyeviti wa Baraza laAardhi na Nyumba la Wilaya wakati wa kikao kazi na maafunzo kinachoendelea mkoani Tanga.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya wakati wa kikao kazi na mafunzo kinachofanyika mkoani Tanga (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

………………………………………………………………..

Na Munir Shemweta, WANMM TANGA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini kuwa waadilifu sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri yanayohusu migogoro ya ardhi.

 Aidha, alizitaka Mamlaka za Nidhamu kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wasiotimiza wajibu wao au wanaoidhalilisha serikali kwa kuendesha vitendo vya rushwa.

Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya nchini pamoja na Wasajili Wasaidizi wanakutana mkoani Tanga kwenye kikao kazi na mafunzo cha siku nne kujadiliana namna bora ya kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma bora kwa wananchi kuhusiana mashauri ya ardhi.

‘’Daima tukumbuke ili mabaraza ya ardhi yaweze kuheshimika ni wajibu wenu wenyeviti wa mabaraza kama watumishi wa umma kufanya kilicho sahihi yaani kuzingatia weledi, kuwa waadilifu  na kuwajibika. Tukumbuke kuwa sisi ni watumishi wa umma ni waajiriwa wa wananchi‘’ alisema Ridhiwani

Akizungumza kwenye kikao kazi na Mafunzo mkoani Tanga tarehe 5 April 2022 Naibu Waziri wa Ardhi alisema, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kama vyombo vya kutoa haki yana wajibu wa kuhakikisha yanatoa huduma bora kwa wananchi ili kuondoa malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa maadili katika kushughulikia migogoro ya ardhi.

‘’Haki na wajibu ni sawa na chanda na pete katika uwajibikaji wa daraja la juu. Mtekelezaji wa utoaji au usimamizi wa halki bila kuwa muadilifu ni mtihani mkubwa’’ alisema Ridhiwani.

Alieleza kuwa, maadili ni kitu muhimu cha kuzingatia katika utendaji kazi hasa kipindi hiki ambacho serikali ya wamu ya sita inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanazingatia maadili yanayosimamaia utumishi wa umma.

‘’Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika matamshi yake, mbalimbali ameonesha wazi nia yake ya kuurejesha utumishi wa umma kuwa utumishi uliotukuka na unaozingatia taratibu za utendaji na maadili yanayoongoza utumishi wa umma’’ alisema Ridhiwani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, Wizara yake itaanza kuweka mfumo wa ufuatiliaji utendaji kazi wa wenyeviti wa mabaraza ya ardhi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

‘’Katika mfumo huo wa ufuatiliaji wale wenyeviti ambao utendaji wao utaridhisha tutakuwa pamoja na wale wasiotaka kubadilika itabidi watupishe na tutafute watendaji au wenyeviti walio tayari kutekeleza majukumu na wako tayari kutenda haki na watanzania wote bila kubagua lakini kikubwa zaidi kuwa tayari kubadilisha taswira ya wizara ya kiutendaji kutoka wizara ya malalamiko na kuwa wizara yenye kupewa sifa nzuri za utendaji’’ alisema Dkt Kijazi.

Naye Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini Stella Tullo alielezea mafunzo waliyoyapata wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi nchini alisema kuwa, yatawajengea uwezo na anaamini mara baada ya kujifunza watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi watakuwa na nafasi nzuri ya kusikiliza mashauri ya ardhi sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

About the author

mzalendoeditor