Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ALITAKA JESHI LA MAGEREZA KUTUMIA NGUVU KAZI YA WAFUNGWA KATIKA KUZALISHA

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Magereza pamoja na Wananchi mara baada ya kuweka Mawe ya Msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza Makao Makuu Mkoani Dodoma leo tarehe 25 Machi, 2022.

………………………………………….

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Magereza na majeshi mengine ya ulinzi na usalama kuwa na mashirika ya uchumi na kuwapa wataalamu kutoka nje ya jeshi kuendesha na kusimamia biashara kwa kuingia mikataba na sekta binafsi. 

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akihutubia hafla ya kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi minne katika makao makuu ya Jeshi la Magereza, iliyofanyika Jijini Dodoma.

Aidha, Rais Samia amewaagiza kutumia nguvu kazi ya jeshi kuwashirikisha kikamilifu wafungwa katika kufanya kazi za uzalishaji ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea watakapotoka gerezani.

Rais Samia amesema, yapo magereza 129 katika maeneo mbalimbali nchini hivyo kila gereza likiwa na shughuli kubwa ya uzalishaji, Jeshi la Magereza litaweza kujitegemea na kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa. 

Miradi ya Jeshi la Magereza iliyozinduliwa ni pamoja na nyumba 52 za watumishi zilizogharimu shilingi Bilioni 2.8 kwa ajili ya familia 79 na kiwanda cha kisasa cha samani kilichogharmu shilingi Bilioni 2.

Pia, Rais Samia ameweka mawe ya msingi kwenye kituo maalum cha biashara kilichogharimu shilingi Bilioni 1.75 na hospitali ya kanda ya Jeshi la Magereza itakayogharimu kiasi cha Bilioni 1.36.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) pamoja na vyombo vingine kuangalia kesi ambazo zimekosa ushahidi ili kupunguza msongamano na idadi ya wafungwa mahabusu.

About the author

mzalendoeditor